Habari MsetoSiasa

Wazee walaani serikali kumtesa Miguna

January 9th, 2020 2 min read

Na GEORGE ODIWUOR

KUNDI la wazee wa jamii ya Waluo limeitaka serikali kukoma kumhangaisha wakili Miguna Miguna, ambaye amekwama Uropa baada ya kuzuiliwa kusafiri kurudi nyumbani Kenya.

Wazee hao wakiongozwa na Mzee Nyandiko Ongadi na Walter Ambasa, walieleza kukerwa na namna serikali imekuwa ikimuhangaisha Dkt Miguna.

Bw Ongadi aliitaka serikali kutangaza msimamo wake kuhusiana na kurejea kwake nchini.

“Kumkataza Miguna kuja Kenya ni kukiuka haki zake za kimsingi. Hafai kuendelea kuhangaika katika mataifa ya kigeni,” akasema Mzee Ongadi alipokuwa akihutubiwa wanahabari jana mjini Kendu Bay katika Kaunti ya Homa Bay.

Alisema kuwa Dkt Miguna alizaliwa nchini Kenya hivyo hafai kuzuiliwa kuja nyumbani.

Bw Miguna alisafirishwa kwa nguvu na serikali ya Kenya hadi nchini Canada mnamo Februari 2018 siku chache baada ya ‘kumwapisha’ kinyume cha sheria kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuwa ‘rais wa wananchi’.

Dkt Miguna alisafirishwa, kwa mara ya pili, hadi Canada mnamo Machi 29, 2018 baada ya kuzuiliwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa saa 72.

Desemba 2018, mahakama iliagiza serikali kumlipa Miguna fidia ya Sh7 milioni kwa kumhangaisha bila hatia.

Jaji Chacha Mwita pia aliagiza arejeshewe paspoti yake iliyotwaliwa na serikali alipofurushwa kwa nguvu.

Wakili huyo alikuwa amepanda kuwasili nchini Jumanne wiki hii akitumia ndege ya shirika la Lufthansa lakini akazuiliwa kuendelea na safari alipowasili nchini Ujerumani.

Alizuiliwa kuabiri ndege kuja humu nchini baada ya serikali ya Kenya kutoa ilani ikisema kuwa hatakiwi nchini.

Jaribio lake la kutaka kutumia ndege ya Ufaransa ya Airfrance lilitibuka pale alipoondolewa ndani ya ndege hiyo muda mfupi kabla ya kupaa.

Shirika la Air France lilisema kuwa lilipokea agizo kutoka kwa serikali ya Kenya iliyotishia kuzuia ndege hiyo kutua katika uwanja wa JKIA endapo ingembeba Dkt Miguna.

Serikali ingali inasisitiza kuwa wakili huyo ni sharti atume maombi katika ubalozi wa Kenya apewe paspoti mpya.

Wazee wa jamii ya Waluo walimtaka kinara wa ODM Raila Odinga kumsihi Rais Uhuru Kenyatta ili aruhusu Miguna kurejea humu nchini.

Mzee Ongadi alisema kuwa wakili Miguna hana nia ya kutatiza amani ambayo Wakenya wanafurahia tangu Rais Kenyatta kukubali kufanya kazi na Bw Odinga.

“Mwafaka wa kisiasa baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga unafaa kuwanufaisha watu wote. Dkt Miguna ni miongoni mwa watu wanaofaa kunufaika na handisheki badala ya kuhangaishwa,” akasema.