Habari MsetoSiasa

Wazee walaani ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’

May 12th, 2019 2 min read

Na JOSEPH WANGUI

WAZEE wa jamii ya Agikuyu sasa wanataka makundi ya kisiasa ndani ya chama cha Jubilee yavunjwe huku wakikariri msimamo wao wa awali kwamba Naibu Rais William Ruto hatapata uungwaji mkono wa moja kwa moja kutoka jamii hiyo 2022.

Huku wakilaani kubuniwa kwa makundi ya ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’, wanachama wa baraza la wazee wa jamii hiyo (KCE) waliwataka wanachama wa makundi hayo kusitisha shughuli zao na kampeni za urais na badala yake waelekeze juhudi zao kuimarisha hali ya kiuchumi ya wananchi.

Wakiwahutubia wanahabari Jumapili mjini Nyeri, wazee hao walisema hawataunga mrengo wowote, kati ya hiyo miwili, kwani kila mmoja unawagonganisha Wakenya.

“Hatujihusishi na mitazamo ya kisiasa na kundi linalojiita ‘Kieleweke’ au lile la ‘Tangatanga’. Tunaunga mkono Rais na Serikali yake. Kwa hakika wakati huu wote tumekuwa tukipinga shughuli za mirengo hii,” akasema naibu mwenyekiti wa KCE Peter Njogu Githinji akizungumza na wanahabari katika jumba la Umoja Chambers.

Baraza hilo pia liliunga mkono kauli ya awali ya naibu mwenyekiti wake David Muthoga kwamba ndoto ya urais ya Dkt Ruto haitaungwa mkono wa moja kwa moja kutoka kwa jamii ya Mlima Kenya mwaka 2022.

“KCE inawatambua Rais na naibu wake. Tunaunga mkono Kamati ya Maridhiano kama njia ya kuleta amani na uwiano nchini. KCE pia inaunga mkono Rais katika vita dhidi ya ufisadi. Tumeridhishwa na uongozi wa Bw Muthoga hapa Nyeri na Kenya kwa jumla,” akasema Bw Githinji.

Mwezi uliopita, Bw Muthoga alienda kinyume na ahadi ya Rais Kenyatta aliyotoa kabla ya 2013 na 2017 ya kuunga mkono azma ya Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022 akisema si lazima kwa jamii hiyo kuheshimu ahadi hiyo. Alisema baraza hilo la wazee halikuwa na habari zozote kuhusu uwepo wa makubaliano kati ya wawili hao ambayo yalipaswa kuheshimiwa na jamii za Wakikuyu na Wakalenjin.

“Dkt Ruto anapaswa kuanza mazungumzo mapya na jamii yetu ikiwa anataka imuunge mkono 2022. Kwa sasa asitarajie uungwaji mkono wa moja kwa moja.”