Habari Mseto

Wazee walalamika kutolipwa pesa za uzeeni mwaka mzima

January 3rd, 2020 2 min read

Na SAMUEL BAYA

WAZEE waliokuwa wakipokea mgao wao wa pesa za uzeeni kutoka kwa serikali ya kitaifa sasa wanataka mpango huo uendelezwe.

Baadhi yao katika eneo la Salgaa, kaunti ndogo ya Rongai, Nakuru wanadai ni karibu mwaka mmoja sasa tangu wapokee pesa hizo, ilhali serikali haijawatangazia kama mpango huo umesitishwa.

Wazee kote nchini walikuwa wamesajiliwa kupokea Sh2,000 kila mwezi, lakini sasa wanaishi kwa dhiki.

Wakiongea na Taifa Leo, wazee hao walisema bado hawajajua ni kwa nini serikali imekosa kuwalipa pesa hizo ambazo walidai ni haki yao kikatiba.

Mmoja wa wazee hao, Simon Long’ole aliye na umri wa miaka 73 aliambia waandishi wa habari kwamba, alisajiliwa katika mradi huo miaka miwili iliyopita kupokea Sh2,000 kila mwezi.

“Lakini ilipofika Novemba 2018, mpango huo ulisimamishwa kwa sababu kila nikienda Nakuru mjini kutafuta pesa hizo ninaambiwa hazipo. Nimezunguka kwa mwaka wote ulioisha,” akasema.

Na huku akionyesha ghadhbu yake dhidi mpango huo wa Inua Jamii, Mzee huyo alisema kuwa anaidai serikali kiasi cha Sh20,000.

“Tulianza vizuri lakini ilipofika katikati, mambo yakasimama na hivi tunavyoongea, ninadai Sh20,000 ambazo ni haki yangu. Hatujajua pesa inapotea wapi kwa sababu serikali kila mara inasema kwamba pesa zinatumwa,” akasema Mzee huyo.

Maoni yake yaliungwa mkono na Mzee Stanley Kiptanui ambaye pia ni mzee wa kijiji hicho cha Baraka Community.

Alisema kuwa walisajiliwa mnamo 2016 katika afisi ya chifu wa Salgaa na wakaendelea kupata pesa hizo za wazee kabla ya kusimamishwa.

“Mnamo Novemba 2018 ndipo pesa ziliposimamishwa hadi leo. Tumezunguka katika afisi za serikali na kila mara tukienda benki kuulizia, wanasema pesa bado hazijaletwa,” akasema.

Yeye pia alitilia shaka kwamba huenda pesa hizo zinaingia katika mifuko ya watu wengine kwa sababu wao kama walengwa hawajapata kwa mwaka mmoja sasa.

“Hatujui hii pesa ya wazee inamalizikia wapi kwa sababu kila tukienda benki wanatuambia pesa hakuna tusubiri. Hali hii mpaka lini,” akahoji.

Jina lakosekana

Naye Wesley Kibet ambaye ana ulemavu wa miguu alisema kuwa wakati mpango huo ulianzishwa eneo la Rongai, alikuwa mmoja wa wale ambao walijisajili. Hata hivyo baada ya muda wa kukosa fedha, aliamua kwenda kuulizia kulikoni lakini akaambiwa jina lake haliko.

“Nilirudi huko hata hivi majuzi kuuliza kama jina langu lilionekana katika sajili ya wanaolengwa na serikali lakini nikaambiwa jina langu haliko. Na kwamba nisajiliwe upya. Ninapitia changamoto nyingi kwa sababu mimi ni mlemavu na niko na watoto ninaosomesha,” akasema Bw Kibet.

Hata hivyo akiongea na ‘Taifa Leo’ kwa simu, mratibu wa shughuli za serikali katika eneo la Bonde La Ufa Bw George Natembeya alisema hajapata lalama zozote kutoka eneo la Rongai kuhusiana na jambo hilo.

“Ndio kwanza ninasikia kutoka kwako. Kile ambacho ninajua ni kuwa mgao wa wazee kutoka kwa serikali umekuwa ukiendelea na sijpatiwa ripoti yoyote kuhusu jambo hilo. Ila kwa sababu ni suala ambalo limeibuka, nitafuatilia,” akasema Bw Natembeya.