Habari Mseto

Wazee walia kunyimwa hela za uzeeni

November 10th, 2019 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

WAZEE kutoka vijiji vilivyoko ndani ya msitu wa Boni na vile vya mpakani mwa Kenya na Somalia wameilalamikia serikali kwa kukosa kuwaandikisha ili kupata fedha za uzeeni.

Baadhi ya wazee ambao tayari walisajiliwa kwenye mpango huo aidha wanaililia serikali kwa kufeli kuweka miundomsingi mwafaka ya kuhakikisha wanapokea fedha hizo.

Serikali ya kitaifa ilianzisha mpango huo wa kuwapa pesa za kila mwezi wazee wa miaka 70 na zaidi nchini ili kuwasaidia kujikimu maishani na kuinua jamii kwa jumla.

Wakizungumza na wanahabari kwenye vijiji vya Bodhei, Bar’goni, Milimani, Mangai, Mararani, Kiangwe, Ishakani, Kiunga na Madina, wazee hao walisema ipo haja ya serikali kuhakikisha kila mmoja wao anaandikishwa ili kupata mgao huo wa fedha za uzeeni.

Pia waliitaka serikali kuhakikisha fedha hizo zinatolewa kwenye maeneo yao badala ya kuwataka wazee hao kusafiri hadi kwenye sehemu za mbali kupokea fedha hizo.

Bw Ajo Hussein Gurba, mkazi wa Bodhei, alisema licha ya kuandikishwa kwenye mpango huo wa fedha za uzeeni, mara nyingi amekuwa akikosa kupokea fedha hizo kutokana na changamoto za usafiri.

Bw Ajo Hussein Gurba wa kijiji cha Bodhei ndani ya msitu wa Boni. Ni miongoni mwa wazee wanaoteseka kwa kukosa fedha za uzeeni. PICHA/ KALUME KAZUNGU

Wazee wa kijiji cha Bodhei na viungani mwake huhitajika kusafiri hadi kijiji cha Bar’goni ambacho kiko umbali wa takriban kilomita 25 ili kupokea fedha hizo.

Wengine pia hulazimika kusafiri kutoka vijijini mwao hadi miji ya Mokowe au Lamu ambayo ni zaidi ya kilomita 50 ili kupokea fedha hizo.

“Kutoka Bodhei mpaka Bar’goni au Lamu utatumia nauli ya hadi Sh 1800 ilhali pesa unazofaa kupokea ni Sh 2000 pekee. Barabara zetu ni mbaya kwani hazipitiki kutokana na ati ati za kiusalama. Isitoshe, mafuriko ya hivi majuzi yameharibu kabisa barabara zetu. Tumekosa kupokea fedha hizo za uzeeni kwa zaidi ya miezi mitano sasa. Serikali itufikirie,” akasema Bw Gurba.

Bi Khadija Baraka alisema ni vyema serikali kubadili mfumo wa kuwapokeza wazee fedha hizo, ikiwemo kutumia njia ya simu ili iwe rahisi kwao kufikiwa na mgao wa fedha hizo za kila mwezi.

Pia aliitaka serikali kuendeleza usajili wa wazee kila mara kwani wengi wa wazee waliofikisha miaka 70 na zaidi bado hawajasajiliwa kupokea fedha za serikali.

“Mfumo wa kupokea fedha ubadilishwe. Badala ya sisi kusafiri hadi Lamu ili kupokea fedha hizo kutoka kwa benki, itakluwa bora zifikishwe milangoni mwetu. Siku hizi kuna simu za rununu. Kwa nini wasitumie njia ya Mpesa kutusambazia fedha hizo? Tunateseka sana. Fedha hatuzipati,” akasema Bi Baraka.

Bw Omar Abdalla alisema haelewi sababu inayopelekea baadhi yao kukosa kupokea fedha hizo licha ya kuhitimu umri unaostahili wao kuanza kupokea mgao huo.

“Nimeandikishwa kitambo na nimekuwa nikihangaika kwenda benki lakini cha kushangaza ni kwamba sijaweza kupokea fedha hizo. Kila nikienda benki ninaambiwa fedha zimechelewa. Sitaki kuandikishwa wala kuhesabiwa na mtu. Hakuna faida yoyote,” akasema Bw Salim.