HabariSiasa

Wazee wapanga kuwapatanisha Ruto na Raila

February 3rd, 2020 2 min read

OSCAR KAKAI na WYCLIFF KIPSANG

WAZEE wa jamii ya Wakalenjin wanataka kuwapatanisha Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, huku cheche za maneno kuhusu siasa za urithi wa urais mwaka wa 2022 zikizidi kurushwa.

Wazee hao walio chini ya muungano wa Baraza la Wazee la Myoot, jana walitoa wito pia kwa Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati ili viongozi hao wawili wapatanishwe kwa minajili ya kudumisha amani, umoja na maendeleo ya taifa hili.

Walieleza wasiwasi wao kwamba mizozo kati ya wawili hao inaweza kusababisha uhasama wa kijamii nchini. Mwenyekiti wa baraza hilo, Bw James Lukwo, alisema Rais ana nafasi bora zaidi ya kutuliza ushindani wa kisiasa kati ya Dkt Ruto na Bw Odinga.

Wasiwasi wao umetokea wakati ambapo kuna mjadala mkali kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI) kwani kila upande unapanga mikutano yake ya hadhara kote nchini.

“Tumegundua kwamba mgawanyiko unazidi kutokea kati ya makundi ya kikabila na kisiasa. Hali hii inaongeza uhasama. Pande hizo mbili zinafaa zikubaliane kuhusu jinsi ya kuendesha mikutano ya BBI kitaifa,” akasema Bw Lukwo.

Aliongeza kuwa wazee kutoka jamii za Wakikuyu, Waluo na Wakalenjin wanafaa wajitokeze kueneza umoja kwani nchi hii inaendelea kugawanyika kuhusu BBI.

“BBI ilinuiwa kuleta umoja wa wananchi. Hili litafanikishwa vipi wakiwa bado wanazozana? Tunakosa matumaini kwa Kenya. Tunataka viongozi hao wawili wastaafu kwa amani huku nchi ikielekea upande unaofaa,” wakasema katika taarifa.

Wazee hao waliozungumza mjini Kapenguria walisema taharuki ya kisiasa iliyotanda nchini inavuruga mipango ya maendeleo na utoaji huduma kwa wananchi.

“Sisi kama wazee, hatufurahishwi na yale tunayoshuhudia nchini. Tunatoa wito kwa Rais aingilie kati na kutoa mweleko unaofaa kuchukuliwa. Wewe ndiwe bosi na huu ni wakati wako wa kuchukua hatua. Watazozana hadi lini?” akauliza Bw Lukwo.

Bw Odinga alipata ufuasi mkubwa wa kisiasa mnamo 2007 kwa ushirikiano na Dkt Ruto lakini wawili hao wakakosana baadaye na tangu hapo, wamekuwa mahasimu wakubwa wa kisiasa.

Wandani wa Naibu Rais humlaumu kiongozi huyo wa ODM kwa kutumia kura za jamii ya Wakalenjin alizopata kwa wingi mnamo 2007 kujiinua kisiasa kisha akawasahau, lakini Bw Odinga hukana madai hayo.

Wazee wa jamii ya Wakalenjin walitoa changamoto kwa viongozi wa kisiasa na wafuasi wa vigogo hao wawili wazike tofauti zao na washirikiane kwa manufaa ya Wakenya wanaotegemea uongozi wao. Bw Lukwo alisema viongozi wengi sasa wanatumia muda wao mwingi kuzozana na kushambuliana badala ya kuleta maendeleo.

Wazee hao wamewahi kujaribu kumpatanisha Dkt Ruto na Seneta wa Baringo Gideon Moi aliye pia Kiongozi wa Chama cha Kanu, lakini hawajafanikiwa. Wawili hao huzozania umaarufu wa kisiasa katika eneo la Rift Valley.