Habari

Wazee wataka Uhuru na Ruto wapatane kupunguza joto la siasa nchini

October 9th, 2020 2 min read

STEVE NJUGUNA na CECIL ODONGO

BARAZA la Wazee kutoka Bonde la Ufa limetoa wito kwa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto watatue tofauti zao za uongozi ili kupunguza joto la kisiasa linaloendelea kupanda nchini.

Wazee hao wameonya kwamba ghasia huenda zikazuka tena kutokana na uadui mkubwa kati ya Rais na naibu wake, wakitoa mfano wa kisa cha Murang’a wiki jana ambapo watu wawili walifariki mjini Kenol.

“Joto la kisiasa linaendelea kupanda nchini na litazimwa tu iwapo Rais na naibu wake wataketi chini, wazungumze na kusuluhisha tofauti zao. Nchi hii inaelekea pabaya na viongozi hao wawili wanafaa wapatane,” akasema mwenyekiti wa baraza la wazee hao Gilbert Kabage.

Walikuwa wakizungumza mjini Rumuruti, Laikipia Magharibi wakati wa mkutano wa baraza hilo ambapo walisema kiini cha ghasia za sasa ni uhasama wa kisiasa kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto.

“Tuliwachagua ili kudhihirisha kwamba nchi hii inaweza kukumbatia umoja na amani hasa baada ya mkutano wenu katika uwanja wa Afraha. Ni jukumu lenu wawili kutangaza hadharani kwamba mmekosana ili taifa lisonge mbele,” akaongeza.

Hata hivyo, alisisitiza kwamba wanaunga mkono serikali ya Jubilee mkono na ni wajibu wa Rais na naibu wake kutafuta muafaka kuhusu masuala yanayosababisha wazozane.

“Wakenya huwa na amani viongozi wao wasipofarakana. Tunataka kumwona Rais na Naibu Rais wakiwaunganisha Wakenya,” akasema Bw Kabage.

Mwenyekiti huyo pamoja na wazee wengine pia walitoa wito kwa Rais na Naibu wake wawadhibiti wandani wao wa kisiasa hasa wale wanaoshiriki malumbano makali katika chama cha Jubilee.

Kando na hayo, wazee hao waliwaonya wanasiasa dhidi ya kugawanya Wakenya kwa msingi wa kikabila, wakisema chuki na ghasia za kikabila zimeponza taifa hili mno miaka ya nyuma.

Wakati huo huo, viongozi wa dini ya Kiislamu wameunga mkono msimamo wa Baraza la Kitaifa la Ushauri kuhusu Usalama (NSAC) kwamba wanasiasa wawajibike ghasia zinapotokea katika mikutano yao.

Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Waislamu Nchini (SUPKEM) Hassan Ole Naado, alisema viongozi wanaendelea kupandisha joto la kisiasa nchini kwa kutoa matamshi ya uchochozi na kuelekeza nchi katika mkondo wa ghasia jinsi ilivyokuwa 2007.