Habari Mseto

Wazee wataka wafidiwe kwa hasara iliyosababishwa na mafuriko

October 3rd, 2020 1 min read

Na JOSEPH WANGUI

KUNDI la wazee 91 kutoka jamii ya Ilchamus katika Kaunti ya Baringo, limewasilisha kesi mahakakani likitaka fidia kutoka kwa Serikali kwa hasara iliyokadiriwa na wakazi kutokana na mafuriko yaliyoshuhudiwa baada ya Ziwa Baringo kuvunja kingo zake.

Katika kesi hiyo ambayo imeorodheshwa na mahakama kuu ya Nairobi kuwa ya dharura, wazee hao wameishtaki serikali kwa kuwapuuza wakazi wa jamii yao na kukosa kukabiliana vilivyo na mafuriko yaliyozuliwa na wingi wa maji ziwani.

Kupitia kwa wakili Thomas Letangule, jamii ya Ilchamus inataka mahakama kuamuru kuundwa kwa tume ya wataalamu katika masuala ya usimamizi wa umma kutathmini kiwango cha hasara iliyosababishwa na janga hilo.

Kwa mujibu wa Letangule, tume itakayobuniwa itatoa pia mapendekezo yatayohakikisha kwamba haki za wakazi wa jamii ya Ilchamus zinalindwa na wanapokezwa huduma muhimu za serikali kila watakapozihitaji.

“Tume ilenge pia kiwango cha madhara ambayo janga hili limesababishia wakazi na kupendekeza kiasi cha fidia kwa waathiriwa wote. Tunataka korti iamuru kwamba shughuli hiyo ikamilike chini ya kipindi cha siku 60 zijazo,” akasema Letangule.

Kwa kuwa eneo husika limekuwa likishuhudia visa vingi vya mashambulio ya kigaidi na wizi wa mifugo, wazee wanataka tume itakayoundwa chini ya maagizo ya mahakama ifanikishe mipango ya kurejesha amani na utangamano miongoni mwa majirani na jamii ya Ilchamus.

Aidha, wanataka serikali iwape makao wanajamii waliotengwa na jamaa zao kutokana na vita vya kijamii kwa kuwa hilo ni miongoni mwa masuala yanayochangia wizi wa mifugo, vita vya wanajamii wenyewe kwa wenyewe na mashambulio ya kigaidi katika Kaunti ya Baringo.

IMETAFSIRIWA NA: CHRIS ADUNGO