Habari Mseto

Wazee wavalie barakoa aina ya N95, WHO yashauri

June 9th, 2020 2 min read

CHARLES WASONGA na SAMMY WAWERU

SHIRIKA la Afya Ulimwenguni (WHO) limependekeza kuwa wazee wenye umri wa miaka 60 kwenda juu na watu wenye magonjwa sugu wawe wakivalia barakoa aina ya N95 nyakati zote maeneo ya umma.

Hii, shirika hilo linasema, ni kutoka na hali kwamba watu hawa wana kinga ya chini miilini mwao kutokana na uzee au kutokana na magonjwa hayo.

Kwenye kikao na wanahabari Jumatatu, Waziri Msaidizi wa Afya Dkt Rashid Aman alisema kuwa wale wanaowatunza wagonjwa wa Covid-19 chini ya mpango wa kuwatunza nyumbani pia wanahitaji kuvalia maski aina ya N95 wanapowahudumia watu hao.

“Maski aina ya N95 ina kinga zaidi kwa sababu ya namna ilivyotenzwa. Hii ndio maana hutumiwa katika hali ambapo kinga inahitajika; kama wakati ambapo wahudumu wa afya wanawatunza wagonjwa hospitalini. Wagonjwa wanaohudumiwa pia wanapaswa kutumia maski hizi,” akasema Dkt Aman.

Aliongeza kuwa raia wa kawaida wanapaswa kuendelea kuvalia maski zilizotengenezwa kwa njia ya kawaida nyakati zote ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Hata hivyo, Dkt Aman alisisitiza kuwa wazee wenye umri wa miaka 60 kwenda juu wanapaswa kujaribu wawezavyo kukaa nyumbani.

Mnamo Ijumaa WHO iliyataka mataifa ya ulimwengu kuhimiwa raia kuvalia maski katika maeneo ambako kuna uwezekano mkubwa wa virusi vya corona kusambaa.

“Na wahudumu wa afya na wale wanaowatunza wagonjwa wanapaswa kuvalia maski ya kimatibabu nyakati zote wakiwa kazini,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus kwenye kikao na wanahabari jijini Geneva, Uswisi.

“Pili, katika maeneo ambako virusi vya corona vinasambaa katika jamii, tunawashauri watu wenye umri wa miaka 60 kwenda juu au wenye magonjwa sugu, kuvalia maski katika mazingira ambapo hawawezi kutengana na wenzao kwa urahisi,” Tedros akasema.

“Na tatu WHO inahimiza serikali mataifa yahimize umma kuvalia maski nyakati zote katika maeneo ambako ni vigumu kwa watu kutotengana kama vile ndani ya magari ya uchukuzi wa umma, madukani miongoni mwa maeneo mengine,” akaongeza.

Wagonjwa wasioonyesha dalili

Haya yanajiri huku Wizara ya Afya nchini Kenya ikikiri kuwa vituo vya afya vimejaa wagonjwa.

Ongezeko hilo pia limechangia wahudumu wa afya kuzidiwa na kazi.

“Vituo vya afya vimelemewa, vifaa na wahudumu wa afya ni haba ikilinganishwa na idadi kuu ya wagonjwa,” Dkt Aman akasema.

Awali, Wizara ya Afya ilikuwa imedokeza kwamba kutokana na vituo vya afya kuashiria kujaa wagonjwa, itaruhusu baadhi yao kuondoka ili kuchungiwa nyumbani.

Huku pendekezo hilo likizua mdahalo, jinsi wagonjwa wa virusi hatari vya corona watachungiwa nyumbani ikizingatiwa kuwa wengi wao wanapatia changamoto za unyanyapaa, Dkt Aman amesema wanaolengwa ni waliopimwa na kuthibitishwa kuugua ila hawaonyeshi dalili zozote.

Dalili za homa ya corona ni kiwango cha joto cha mwathiriwa mwilini kupanda kuliko cha kawaida, maumivu ya kichwa, kikohozi kizito, matatizo ya kupumua, miongoni mwa zingine, Dkt Aman akieleza kwamba wanaonyesha dalili hizo watalazwa hospitalini.

“Wasioonyesha dalili ndio tunalenga wachungiwe nyumbani,” waziri akasema, akieleza kwamba mikakati maalum itawekwa kufanikisha shughuli hiyo.

Mnamo Jumamosi katika hotuba yake kwa taifa, Rais Uhuru Kenyatta alisema wiki hii atakutana na magavana wote 47 ili kujadili mikakati itakayowekwa na kila kaunti kudhibiti msambao wa Covid-19.

Aidha, Rais alisema kila kaunti inapaswa kuwa na uwezo wa kulaza zaidi ya wagonjwa 300 ili uchumi ufunguliwe kikamilifu.