Habari

37 wazikwa hai

November 24th, 2019 2 min read

Na OSCAR KAKAI na BENSON MATHEKA

  • Novemba 22 2019: Watu watatu wasombwa na maji katika visa viwili tofauti Mbooni, Makuen
  • Oktoba 30 2019 : Watu watatu wasombwa na mafuriko Taita Taveta
  • Oktoba 18 2019: Familia ya watu wanne yazikwa na maporomoko Elgeyo Marakwet
  • Oktoba 17 2019: Watu watatu wasombwa na maji Moyale kaunti ya Marsabit, wawili Mandera na wawili Wajir
  • Oktoba 17 2019: Watu wanne waangamia gari lao liliposombwa na mafuriko Kitui

WINGU la simanzi limetanda Kaunti ya Pokot Magharibi baada ya watu zaidi ya 37 kufariki baada ya maporomoko ya ardhi kuzika vijiji vitatu Ijumaa usiku kufuatia mvua kubwa inayonyesha nchini.

Mkasa huo ulitokea katika vijiji vya Nyarkulian Pokot Kusini, Muino na Parua vilivyoko wilaya ya Pokot ya Kati.
Kamishna wa kaunti hiyo, Bw Apollo Okello alisema miili kumi na mitano ilipatikana kufikia jana alasiri na kwamba, watu 22 hawakuwa wakijulikana waliko.

Rais Uhuru Kenyatta kwenye risala aliyotuma jana alasiri alisema watu 29 waliangamia kwenye mkasa huo.

“Maporomoko hayo yalitokea saa nane na nusu na yamepokonya nchi watu 29 waliothibitishwa kufariki na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali zikiwemo barabara na daraja,” alisema Rais Kenyatta.

Aliagiza idara za serikali zinazohusika na mikasa, wakiwemo maafisa wa jeshi la Kenya, polisi na mipango maalumu kusaidia kuepusha maafa zaidi katika eneo hilo.

Aliagiza Kamishna wa kaunti kuhakikisha walioathiriwa wanapata misaada ya chakula na dawa.

Waliojeruhiwa wakiwemo watoto watatu walipelekwa katika hospitali ya Rufaa ya Kapenguria, huku shughuli za kutafuta miili zaidi iliyoaminika kuzikwa matopeni zikiendelea.

Mvua iliyopitiliza ilinyesha eneo hilo Ijumaa usiku kucha na watu wengi hawakutarajia mkasa ungetokea eneo hilo.

Barabara zote zinazoelekea katika vijiji vya Nyarkulian na Muino ziliharibika kabisa, hali iliyowazuia maafisa wa usalama kufika katika maeneo yaliyoathiriwa kwa haraka.

Bw Okello alieleza kuwa, watu saba wa familia moja walizikwa wakiwa hai katika kijiji cha Nyarkulian, Kaunti Ndogo ya Pokot Kusini huku 17 wakikumbwa na hali kama hiyo katika eneo la Muino, Kaunti Ndogo ya Pokot ya Kati.

Aliongeza kuwa kuna uwezekano watu zaidi walikuwa wamekwama katika matope.

“Tulikabiliwa na ugumu mkubwa kufika maeneo yaliyoathiriwa kwa kuwa barabara zote zimeporomoka. Idadi ya waliofariki inaweza kuongezeka kwani baadhi yao hawajulikani waliko,” alisema.

Vijiji hivyo viko kilomita 70 kutoka Kapenguria, makao makuu ya kaunti hiyo.

Gavana wa kaunti hiyo Profesa John Lonyangapuo na maafisa wa usalama walikwama katika daraja la Mto Muruny katika barabara ya Kitale-Lodwar ambayo sehemu yake iliporomoka walipokuwa wakielekea vijiji vilivyokumbwa na mkasa.

Shughuli za usafiri katika barabara hiyo ziliathiriwa pakubwa.

Chifu wa Kata ya Sonday Bw Joel Bulali alisema, bado wanatafuta miili zaidi. Profesa Lonyangapuo alisema mkasa huo ndio mbaya zaidi kuwahi kulikumba eneo hilo.

Aliomba Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya (KRCS) kusaidia familia zilizoathiriwa kwa mahema, hasa wale nyumba zao zilisombwa na mafuriko.

“Tunahitaji usaidizi kwa kuwa hali inazidi kuwa mbaya; sehemu kubwa ya barabara ya Kitale-Lodwar imeporomoka,” alisema.

Bw Nicholas Kibet, ambaye ni mkazi katika eneo la Muruny, alisema mvua hiyo ilianza mwendo wa saa sita usiku.

“Mvua ilinyesha kwa saa 12 ambapo tulishindwa kutoka katika nyumba zetu. Watu wengi bado hawajapatikana na tunahofia wamefariki,” akasema.

Miili ya waliokufa ilipelekwa katika mochari ya hospitali ya rufaa ya Kapenguria.

Wakati huo huo, idara ya utabiri wa hali ya hewa imeonya kuwa mvua itaendelea kunyesha maeneo tofauti nchini.

Mkurugenzi wa idara hiyo, Stella Aura alisema mvua kubwa itashuhudiwa maeneo ya Kaskazini Mashariki, magharibi na mashariki mwa Rift Valley na Pwani.

Alionya watu wanaoshi maeneo yenye mwinuko na hatari ya maporomoko hasa karibu na milima kuwa waangalifu.