Wazimamoto wafaidika kwa mafunzo ya kisasa

Wazimamoto wafaidika kwa mafunzo ya kisasa

Na KENYA NEWS AGENCY

KIKOSI cha Kukabili Mioto cha Jimbo la Minnesota, Amerika, kimeanza kutoa mafunzo maalum kwa wazimamoto katika Kaunti ya Kisii kuhusu njia za kisasa za kukabili mikasa ya mioto.

Kikosi hicho kinaongozwa na Bw Mark Lynde, huku mafunzo hayo yakiendelea kwa muda wa wiki moja.

Akihutubu katika hoteli moja mjini humo, Bw Lynde alisema anaandamana na kundi la wataalamu wenye tajriba kubwa kuhusu njia za bora za kuzima mioto.

Alieleza kuwa wataalamu hao watawasaidia wazimamoto katika kaunti hiyo kuimarisha ujuzi wao katika kukabili mikasa ya moto.

“Idara ya Kukabili Mioto katika kaunti hii huwa inaendesha vituo 24 vilivyo na zaidi ya wazimamoto 400. Lengo la kuwaleta wataalamu hao ni kuwasaidia kuimarisha na kuboresha ujuzi wao,” akasema.

Bw Lynde alisema kuwa kando na mafunzo, watatoa mchango wa vifaa maalum kuisaidia idara hiyo kuimarisha huduma zake.

Hilo ni kufuatia ombi lililowasilishwa kwao na serikali ya kaunti hiyo.Gavana James Ongwae alikubali kiwa ingawa Kituo cha Kukabili Mioto kilicho mjini Kisii ni miongoni mwa vituo vikubwa zaidi katika eneo hilo, hakina vifaa vya kutosha vya kutoa mafunzo.

Pande hizo mbili zimekuwa zikiendesha mpango wa pamoja kuhusu njia za kukabili mikasa kwa muda wa miaka tisa iliyopita.

You can share this post!

Sera ya wajawazito kuingia darasani ifutwe, walimu warai

Majaji wanaswa