Habari Mseto

Wazir kujua hatima yake Alhamisi

April 11th, 2018 2 min read

Waziri Benson Masubo Chacha (kati) akiwa kortini Aprili 10, 2018 akizungumza na mawakili wakr Edwin Saluny (kushoto) na Job Ngeresa. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAUME anayeshtakiwa kwa madai ya kusajili nambari ya simu ya Mwakilishi Mwanamke wa kaunti ya Murang’a Bi Sabina Chege na kuitumia kuwapunja wabunge wengine pesa atajua hatima yake Alhamisi korti itakapoamua ikiwa ataachiliwa kwa dhamana au la.

Hakimu mkuu Bi Roseline Oganyo aliombwa na mawakili  Job Ngeresa na Edwin Saluny amwachilie Bw Wazir  Benson Masubo Chacha kwa dhamana wakisema anajulikana makazi yake.

Mawakili hawa walisema kuwa mshtakiwa atafika kortini wakati wowote atakapotakiwa.

Lakini kiongozi wa mashtaka Bw Willy Momanyi alipinga ombi hilo akisema atatoroka akiachiliwa kwa vile alikamatwa mjini Tarime nchini Tanzania.

Bw Momanyi alisema mshtakiwa akipatikana na hatia atahukumiwa kifungo cha miaka mitatu kwa kila shtaka. Bi Oganyo atatoa uamuzi kesho ikiwa atamwachilia kwa dhamana.

Mshtakiwa amekanusha mashtaka sita ya kuandikisha nambari ya Bi Chege kwa lengo la kuwapunja umma.

Amekana alijaribu kupokea Sh100,000 kutoka kwa mbunge wa zamani wa Gem Bw Jakoyo Midiwo akidai ametumwa na Bi Chege,

Inspekta John Kiprop kutoka kituo cha Polisi kilichoko Bungeni, alimtia nguvuni Bw Masubo eneo la Tarime nchini Tanzania kabla ya kusafiri hadi nchini Congo.

Wiki iliyopita, mahakama ilikuwa ilitoa kibali cha kumtia nguvuni Bw Masubo kushtakiwa kwa makosa ya kupokea pesa kwa njia ya udanganyifu.

Bi Njagi alifahamishwa kuwa mshukiwa huyo alitiwa nguvuni mnamo Machi 30, 2018 na polisi hawakuwa na muda wa kutosha kumhoji na kuandika taarifa kutoka kwa mashahidi ambao wengi ni wabunge wanawake.

“Naomba hii mahakama imzuilie mshtakiwa katika kituo cha polisi kumhoji na pia taarifa ziandikishwe kutoka kwa Bi Chege na walalamishi wengine aliojaribu kupokea pesa kutoka kwao akitumia jina la mbunge huyo,” akaomba Bw Kiprop.

Lakini wakili Job Ngeresa anayemtetea Bw Masubo alipinga ombi hilo la kuzuiliwa kwa muda wa siku saba.

“Mshukiwa alikamatwa Machi 30, 2018 na amekuwa mikononi mwa polisi,” akasema na kuomba mshukiwa aachiliwe kwa dhamana ili aweze kuenda hospitali kutibiwa, kwa vile anaugua maradhi ya ubongo yajulikanayo kwa lugha ya Kiingereza -Migrane.

“Mshukiwa huyu hakuwa akitoroka bali alikuwa anaenda hospitali ya Muhimbili iliyoko jijini Dar-es-Salaam kupokea matibabu ya kichwa. Mara kwa mara amekuwa akienda nchini Tanzania kusaka tiba ya kichwa kwa vile anapoanza kuugua yeye hutoa nguo akaachwa uchi wa mnyama,” Bw Ngeresa alimweleza hakimu.