Habari Mseto

Wazir kusalia ndani

April 14th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAUME aliyekamatwa kwa madai ya kutumia jina la Mbunge Mwanawake wa kaunti ya Murang’a Bi Sabina Chege kuwatapeli wabunge wengine pesa atasalia ndani hadi afisi ya urekebishaji tabia iwasilishe ripoti kuhusu tabia yake.

Hakimu mkuu katika mahakama ya Citi Bi Rosaline Oganyo aliamuru kesi dhidi ya Bw Wazir  Benson Masubo Chacha almaarufu Sabina Wanjiru Chege  itajwe Aprili 19, 2018.

Mahakama ilisema inataka ripoti kuhusu tabia ya mshtakiwa na pia taarifa za wabunge waliopunjwa.

Hakimu alisema awaamini maafisa wa polisi wanaodai Waziri yuko na tabia mbaya na huenda akatoroka akiachiliwa kwa dhamana.

Polisi walimtia nguvuni mjini Tarime Tanzania akijaribu kutoroka.

Inspekta John Kiprop kutoka kituo cha Polisi kilichoko Bungeni, alimtia nguvuni Bw Masubo eneo la Tarime nchini Tanzania kabla ya kusafiri hadi nchini Congo.

Wiki iliyopita, mahakama ilikuwa imetoa kibali cha kumtia nguvuni Bw Masubo kushtakiwa kwa makosa ya kupokea pesa kwa njia ya undanganyifu.

Bi Njagi alifahamishwa kuwa mshukiwa huyo alitiwa nguvuni mnamo Machi 30, 2018 na polisi hawakuwa na muda wa kutosha kumhoji na kuandika taarifa kutoka kwa mashahidi ambao wengi ni wabunge wanawake.

“Naomba hii mahakama imzuilie mshtakiwa katika kituo cha polisi kumhoji na pia taarifa ziandikishwe kutoka kwa Bi Chege na walalamishi wengine aliojaribu kupokea pesa kutoka kwao akitumia jina la mbunge huyo,” akaomba Bw Kiprop.

Lakini wakili Job Ngeresa anayemtetea Bw Masubo alipinga ombi hilo la kuzuiliwa kwa muda wa siku saba.

“Mshukiwa alikamatwa Machi 30, 2018 na amekuwa mikononi mwa polisi,” akasema na kuomba mshukiwa aachiliwe kwa dhamana ili aweze kuenda hospitali kutibiwa, kwa vile anaugua maradhi ya ubongo yajulikanayo kwa lugha ya Kiingereza -Migrane.

“Mshukiwa huyu hakuwa akitoroka mbali alikuwa anaenda hospitali ya Muimbili iliyoko mjini Dar-es-Salaam kupokea matibabu ya kichwa. Mara kwa mara amekuwa akienda nchini Tanzania kusaka tiba ya kichwa kwa vile anapoanza kuugua yeye hutoa nguo akaachwa uchi wa mnyama,” Bw Ngeresa alimweleza hakimu.