Habari

Waziri Echesa ashauriwa arudi shuleni kunoa maarifa

February 15th, 2018 3 min read

 Na JOHN NGIRACHU na CHARLES WASONGA

Kwa ufupi:

  • Ukakamavu wa Bw Echesa utamfaidi zaidi ikiwa ataanza kujiimarisha kimasomo akiwa kazini
  • Bw Echesa alisema babake alikuwa mchomaji makaa na mamake alikuwa muuzaji wa ndizi
  • Waziri huyu atakuwa akipokea mshahara wa Sh924,000 tofauti na Sh3,000 alizokuwa akipokea zama za kale
  • Anasifiwa kwa kuwezesha Jubilee kupata viti vinane vya ubunge katika eneo la magharibi

Rashid Echesa Muhamed ambaye sasa atahudumu kama Waziri wa Michezo na Turathi ameshauriwa kutumia nafasi hiyo kurejea shule kujiendeleza kimasomo.

Hii ni baada ya wabunge wa Jubilee kuidhinisha uteuzi wake, pamoja na wenzake wanane waliopendekezwa na Rais Uhuru Kenyatta kuwa mawaziri katika kikao kilichosusiwa na wenzao wa NASA.

Akishiriki mjadala kuhusu ripoti ya kamati ya uteuzi iliyomwidhibisha Bw Echesa, na wenzake wanane, mbunge wa Yatta Charles Kilonzo alisema huenda mawaziri wakahitajika kuwa na shahada za digrii siku zijazo.

“Nilifurahishwa na namna Bw Echesa alivyojibu maswali mbele ya kamati ya uteuzi lakini anafaa kurejea shuleni kwa sababu huenda sheria ikabadilishwa siku moja na watakaoteuliwa mawaziri kuhitajika kuwa na shahada za digrii,” akasema Bw Kilonzo.

Bw Kilonzo, ambaye ni mbunge huru, alieleza kuwa ukakamavu wa Bw Echesa utamfaidi zaidi ikiwa ataanza kujiimarisha kimasomo akiwa kazini.

Lakini kiongozi wa wengi Aden Duale alisema uhitimu wa kimasomo siyo hitaji kuu kuliko uwezo wa mtu kutekeleza majukumu ya uwaziri.

“Kazi ya uwaziri haina uhusiano wowote na shahada za digrii au chuo kikuu ambacho mtu alisomea bali uwezo wake wa kutekeleza majukumu aliyopewa,” akasema Bw Duale.

Katiba haijafafanua kuhusu kiwango cha masomo ambacho mtu anafaa kuwa nacho kabla ya kuteuliwa waziri.

Ripoti ya kamati ya uteuzi inamweleza waziri huyo mteule kama “mwenye umri wa chini zaidi na mkakamavu zaidi” na aliyesoma katika Shule ya Msingi ya Shibale kati ya mwaka wa 1990 na 1997.

Bw Rashid Echesa akielezea kamati ya bunge iliyomhoji kuhusu changamoto alizokumbana nazo kuanzia utotoni mpaka akaamua kujiunga na siasa. Picha/ Hisani

Changamoto tele

Hata hivyo, kutokana na changamoto za kulipa karo hakuweza kuendeleza masomo yake, kulingana na ripoti hiyo ambayo ilitolewa na Spika wa Bunge Justin Muturi.

Alipofika mbele ya kamati hiyo Ijumaa iliyopita, Bw Echesa alisema babake alikuwa mchomaji makaa na mamake alikuwa muuzaji wa ndizi.

Kulingana naye, wakati mwingine mamake alilazimika kutembea kilomita sita hadi sokoni kuuza ndizi.

“Kutokana na kuwa nilizaliwa katika familia yenye watoto wanane, hali ilikuwa ngumu kwangu kwani mamangu na babangu walikuwa wanasumbuka sana kutulea na walishindwa hata kutulipia karo,” akasema.

 

Kazi ya kupakia

Baada ya kusitisha masomo yake ghafla, Bw Echesa alitafuta kibarua katika Kampuni ya Sukari ya Mumias ambapo alipata kazi ya kupakia magunia ya sukari kwa malori.

Ni wakati alipokuwa Mumias ambapo aliingilia ndondi chini ya Klabu ya Ndondi ya Mumias.

Bw Echesa ambaye anatoka katika ukoo wa Nabongo ulioongozwa na Mumia Nabongo, alipanda daraja katika ndondi hadi akafikia daraja la Kenya Open.

“Baadaye niliandamwa na aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya magereza Bw Gichuki, ambaye aliniambia angependa nijiunge na timu yake. Kutokana na kuwa maisha yalikuwa magumu, wazazi wangu walishindwa hata kulipia ndugu zangu karo, niliamua kujiunga na kikosi cha magereza,” akasema.

Mwanamume huyo sasa akiidhinishwa kuwa waziri atakuwa akipokea mshahara wa Sh924,000 tofauti na Sh3,000 alizokuwa akipokea zama hizo za kale.

Bw Rashid Echesa aliyeidhinishwa na bunge kusimamia Wizara ya Michezo.  Yeye ni miongoni mwa watu wanaosifiwa kwa kuwezesha Jubilee kupata viti vinane vya ubunge katika eneo la Magharibi. Picha/Maktaba

Alitumia PNU kujenga umaarufu

Bw Echesa alieleza kuwa alivutiwa kuingilia mambo ya kisiasa katika mwaka wa 2007 alipokuwa nyumbani akipumzika baada ya kuoa, wakati alipomsikia jirani akimwambia mamake kuhusu mkutano wa Chama cha PNU.

Alisikia chama hicho cha Mwai Kibaki kilikuwa kikitafuta mtu wa kusimamia shughuli zake na akajiamini kwamba kutokana na alivyokuwa mashuhuri miongoni mwa vijana, angefanya kazi hiyo ipasavyo.

Kocha wake alimruhusu ajiunge na siasa na akachaguliwa kuwa mratibu wa PNU katika eneo la Mumias.

Alijisifu kwamba licha ya kuwa chama hicho hakikuwa maarufu magharibi, aliyekuwa rais Kibaki alifanikiwa kupata kura 18,000.

Katika mwaka wa 2008, alijiunga na ODM ambapo alichaguliwa kuwa kiongozi wa vijana kitaifa lakini akahamia mrengo wa serikali mwaka wa 2016.

Yeye ni miongoni mwa watu wanaosifiwa kwa kuwezesha Jubilee kupata viti vinane vya ubunge katika eneo la magharibi.