Habari MsetoSiasa

Waziri alaumiwa kwa mimba za wanafunzi

November 7th, 2018 1 min read

ONYANGO K’ONYANGO na SHABAN MAKOKHA

BAADHI ya viongozi wa kisiasa sasa wanamlaumu Waziri wa Elimu Amina Mohamed kwa ongezeko la visa vya wanafunzi kupachikwa mimba katika maeneo mbalimbali nchini.

Wabunge hao wanamtaka waziri kueleza ni kwa nini wanafunzi wanatungwa mimba wakiwa shule, mahala ambapo wanapaswa kuwa wamelindwa.

Wakiongozwa na Seneta wa Nandi Samson Cherargei, viongozi hao walimkashifu waziri huyo kwa kile walichodai ni kushindwa kubuni sera dhabiti ili kukabili visa hivyo vinavyotishia mustakabali wa wanafunzi wengi.

Bw Cherargei alisema idadi ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kitaifa wa shule za msingi (KCPE) wakiwa na mimba na wengine wakijifungua ni ya kushtusha mno na inapaswa kusukuma serikali kuchukua hatua kali kukomesha visa hivyo.

“Waziri Amina anapaswa kutueleza wazi kwa nini wasichana wetu wanapata mimba shuleni badala ya kupewa elimu. Sharti adhabu kali ichukuliwe kwa wanaohusika wakiwemo wazazi ambao wanachangia kuwepo kwa visa hivyo,” alisema Bw Cherargei.

Seneta huyo alisema bunge litabadilisha sheria ya dhuluma za kimapenzi ili washukiwa waachiliwe kwa bondi ya Sh1 milioni badala ya kiasi cha sasa cha Sh100,000.

Naye mbunge wa Kesses Swarup Mishra alimtaka Waziri Mohamed kuhakikisha masomo kuhusu ngono na mahusiano ya kimapenzi yameanza kufunzwa shuleni.

Mbunge wa Cherang’any Joshua Kuttuny alisema Wizara ya Elimu inapaswa kuhakikisha shule zote ni za malazi ili kupunguza visa vya wanafunzi kushawishiwa kushiriki ngono.

Kwingineko, Kamishna wa Kaunti ya Kakamega Jaldesa Abdulrizak amepiga marufuku densi za usiku almaarufu ‘disco matanga’, ambazo zimelaumiwa kwa ongezeko la mimba za wanafunzi.

Kwenye mtihani wa KCPE uliokamilika wiki iliyopita na ule unaoendelea wa KCSE, kumeripotiwa idadi kubwa ya watahiwa kujifungua.

Katika Kaunti ya Kilifi pekee kumeripotiwa kuwa wanafunzi zaidi ya elfu 13 wamepata mimba kwa mwaka mmoja