Michezo

Waziri Amina aomboleza kifo cha mamake Paul Tergat

September 24th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAZIRI wa Michezo Amina Mohamed ametuma risala za rambirambi kwa Rais wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya (NOC-K) Paul Tergat kufuatia kifo cha mamaye Esther Toyoi Kipkuna mapema Septemba 23.

“Alikuwa mama muangalifu, asiye na ubinafsi na mwenye huruma na ambaye alilea Dkt Paul (Tergat) na watoto wake wote akiwapatia ushauri mzuri na mwelekeo mwema.

“Kwa niaba yangu na Wizara ya Michezo na wanamichezo wote, naungana na familia yake kuombea Paul Tergat na familia yake yote rehema za Mwenyezi Mungu iweze kustahimili wakati huu mgumu,” alisema waziri huyo kupitia mtandao wake wa Twitter.

Hapo Jumatano, NOC-K ilivunja habari za kifo cha mamake Tergat ikisema kuwa Mama Esther alifariki akipokea matibabu katika hospitali ya Mediheal mjini Nakuru.

Kaimu Katibu wa NOC-K, Francis Mutuku alitaja kifo hicho kuwa pigo kubwa kwa familia ya Tergat, ambayo ilikuwa pia imepoteza mama mkwe.

Afisa huyo pia alisema kifo hicho kitaathiri mipango ya NOC-K iliyokuwa ikiweka juhudi za kurejelea michezo kwani “Tergat na Kamati Kuu ya NOC-K wamekuwa katika mstari wa mbele katika kuona michezo inarejelewa chini ya masharti ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona”. Mipango ya mazishi bado haijatangazwa.