Habari

Waziri anayekaidi Rais

October 26th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA na WANDERI KAMAU

HATUA ya Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri Alhamisi ya kujihusisha wazi na kundi la ‘Tangatanga’ ambalo limekuwa likipinga handisheki na Jopokazi la Uwiano (BBI), inaibua maswali kuhusu uaminifu wake kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Bw Kiunjuri aliungana na wabunge wanaoegemea vuguvugu hilo linalomuunga Naibu Rais William Ruto kutangaza kuwa watapinga ripoti ya BBI ikiwa haitapendekeza usawa katika uwakilishi kwa kutegemea idadi ya watu.

Ikizingatiwa kuwa Bw Kiunjuri aliteuliwa na Rais Kenyatta ambaye ametangaza kwamba ataunga na kutekeleza kikamilifu mapendekezo ya ripoti ya BBI, kuungana na wanaoipinga kunachukuliwa kama kukaidi mkubwa wake.

Rais Kenyatta aliteua Jopokazi lililoandaa ripoti hiyo baada ya muafaka wake na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kwa lengo la kuunganisha Wakenya.

Wiki jana, Rais aliapa kuwa atatekeleza ripoti hiyo kikamilifu liwe liwalo ili kuacha Wakenya wakiwa wameungana atakapostaafu. Akiwa mmoja wa wandani wa Rais, ilitarajiwa kuwa Bw Kiunjuri angeunga hatua ya Rais.

Hata hivyo, alikuwa mmoja wa waliotia saini taarifa iliyosomwa na wanachama wa ‘Tangatanga’ bungeni Alhamisi kuapa kupinga ripoti ya BBI ambayo itakabidhiwa rasmi Rais Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga wakati wowote.

Kinaya ni kwamba, waziri huyo amekuwa mshirika wa karibu wa Rais Uhuru Kenyatta kwa muda mrefu kiasi cha kudaiwa kuwa hakumchukulia hatua wizara yake ilipohusishwa na madai ya matumizi mabaya ya pesa.

Rais Kenyatta ndiye alimrai Bw Kiunjuri kutowania ugavana katika Kaunti ya Laikipia mnamo 2013, kwa ahadi ya kumpa wadhifa serikalini ili awe “mtetezi wake katika siasa za kitaifa.”

Rais alimteua Waziri wa Ugatuzi mnamo Novemba 2015 baada ya Gavana wa Kirinyaga, Bi Anne Waiguru kujiuzulu kutokana na tuhuma za ufisadi zilizolikumba Shirika la Kitaifa la Huduma za Vijana (NYS) ambapo karibu Sh791 milioni zilipotea katika hali tatanishi.

Baada ya kuanza kipindi cha pili mnamo 2017, Rais alimhamishia katika Wizara ya Kilimo.

Rais Kenyatta alikosa kumchukulia hatua Bw Kiunjuri mwaka uliopita baada ya wizara yake kujipata katika kashfa ya kuwalipa wakulima ghushi wa mahindi Sh1.8 bilioni katika hali ya kutatanisha.

Licha ya waziri huyo kushindwa kueleza taratibu ambazo zilitumika kuwalipa wakulima hao, Rais Kenyatta alitoa onyo tu, bila kumchukulia hatua yoyote.

“Naapa mbele ya Mungu, jaribu kufanya hivyo tena. Utaona yatakayokufika. Sisi hatutaki mchezo tena…Mungiriha ni mukuona (Mkilipa tena mtajuta),” akamwonya Rais Kenyatta hadharani kwa lugha ya Gikuyu mnamo Oktoba mwaka uliopita kwenye Maonyesho ya Kilimo ya Nairobi.

Mnamo Machi mwaka huu, Rais Kenyatta pia alimkosoa Bw Kiunjuri hadharani na mawaziri wengine wawili nchini Namibia kwa “kutonakili aliyokuwa akieleza.”

Usaliti

Licha ya onyo kama hilo, Bw Kiunjuri amekuwa akizuru maeneo mbalimbali nchini akimpigia debe Dkt Ruto, huku akiwatahadharisha wenyeji wa Mlima Kenya dhidi ya kumsaliti.

Kwenye hotuba zake, waziri amekuwa akitumia mafumbo na semi kutokana na ufahamu wake mkubwa wa lugha ya Kikikuyu, akisema jamii za Mlima Kenya zinapaswa “kurudisha mkono” kwa Dkt Ruto, kwa kuonyesha uzalendo wa Rais Kenyatta.

“Wema hulipwa kwa wema. Haiwezekani kwa rafiki kukutoa katika makucha ya chui na kumwacha rafiki huyo kuliwa na chui huyo,” alisema waziri mnamo Julai alipohutubu katika eneobunge la Dagoretti jijini Nairobi.

Wadadisi wanasema inashangaza licha ya Rais kutomchukulia hatua, anaenda kinyume na maamuzi yake kuhusu BBI.

“Si kawaida kwa Waziri kukaidi wazi maagizo yanayotolewa na Rais kuhusu kushiriki kwenye siasa. Hafanyi hivyo bila kufahamu nia hiyo,” asema Profesa Macharia Munene, ambaye ni mdadisi wa siasa na kukiri kuwa Rais Kenyatta anamwamini waziri huyo.

Mnamo Juni, ghasia ziliibuka katika eneobunge la Nyeri Mjini, baada ya vijana kuvamia hafla aliyohudhuria Bw Kiunjuri wakimtaja kuwa mwanachama wa ‘Tangatanga’.

Bw Kiunjuri alikuwa akitekeleza majukumu yake kama waziri wakati ghasia hizo zilizuka.