Waziri apongeza Lionesses kujikatia tiketi ya fainali ya Zoni ya Tano

Waziri apongeza Lionesses kujikatia tiketi ya fainali ya Zoni ya Tano

Na GEOFFREY ANENE

WAZIRI wa Michezo Amina Mohamed amepongeza Kenya Lionesses kwa kupiga wenyeji Rwanda 79-52 katika nusu-fainali ya mashindano ya mpira wa vikapu ya Afrika ya Zoni ya Tano jijini Kigali mnamo Julai 16.

“Mmefaulu! Hongera Lionesses kwa kushinda mechi ya nusu-fainali dhidi ya Rwanda. Tunawashangilia. Leteni hilo taji nyumbani kesho (Julai 17)!” Alisema waziri huyo.

Lionesses ya kocha George Mayienga, ambayo ilipoteza 77-45 dhidi ya Rwanda katika raundi ya kwanza, ilionyesha nia yake ya kuzima wenyeji hao mapema iliposhinda robo ya kwanza kwa alama 25-11. Ilienda mapumzikoni ikiwa imefungua mwanya wa alama 19 ilipoongoza 42-23.

Nahodha Melissa Akinyi alifungia Kenya pointi nyingi (21). Wafungaji wengine wa Lionesses walikuwa Victoria Reynolds (pointi 16), Felmas Koranga 12), Mercy Wanyama (9), Rose Ouma (7), Brenda Wasuda (6), Christine Akinyi (5), Natalie Akinyi (2) na Vilma Owino (1). Rwanda ilipata alama nyingi kutoka kwa T. Henderson (22) na B. Murekatete (13).

Mabingwa watetezi Misri walikuwa wa kwanza kujikatia tiketi ya fainali waliponyamazisha washiriki wapya kabisa Sudan Kusini 99-65. Inamaanisha kuwa fainali itakuwa kati ya Kenya na Misri.

Fainali ni Julai 17. Lionesses ilipoteza 107-106 dhidi ya Misri katika mechi ya mwisho ya makundi mnamo Julai 14.

Wakati mmoja Kenya ilikuwa imefungua pengo la alama 25 dhidi ya Misri kabla ya kupoteza mwelekeo na kupoteza. Mshindi wa fainali ya Zoni ya Tano ataingia Kombe la Afrika maarufu kama AfroBasket nchini Cameroon mwezi Septemba.

You can share this post!

MUTUA: Mbona hasira za Wakenya zinaishia kuuana kiafriti?

MWANAMUME KAMILI: Ndoa thabiti ni msingi wa familia na...