Habari MsetoSiasa

Waziri ataka mapasta tapeli wahukumiwe kama wahalifu

September 30th, 2019 2 min read

NA CHARLES WANYORO

WAZIRI Utumishi wa Umma Prof Margaret Kobia Jumapili amependekeza kwamba wahubiri wanaodai kuwa na uwezo wa kuwaombea wanawake ili wapate waume na fedha, wachukuliwe kama wahalifu wanaoendeleza dhuluma za kijinsia.

Prof Kobia alisikitika kwamba tabia hiyo imeongezeka miongoni mwa wahuburi ambao huwahadaa wanawake kwamba ibada takatifu itawapa waume, fedha na hata kuponya maradhi sugu yanayowaandama.

Akizungumza katika uwanja wa Kinoru, mjini Meru wakati wa kugawa hundi kwa makundi ya vijana na wanawake, Prof Kobia alieleza kusikitishwa kwake na hali wanayopitia wanawake ambao hupoteza heshima yao katika jamii na fedha baada ya kutapeliwa.

Aidha, alisema wanawake huogopa kuzungumzia dhuluma mikononi mwa wahubiri au viongozi wa kidini, kwa imani kuwa maombi yao yatakuja kutimia.

Kulingana na Prof Kobia, uwezo wa kiuchumi utawaepusha wanawake wajane na maskini kuingia kwenye mtego wa wahubiri wakora ambao huwanyanyasa.

“Kile ambacho tunawaomba wanawake ni kuwa wainuke ili wawe na uwezo wa kiuchumi ambao utawasaidia kuwasomesha wanao au kuwapa huduma bora za kimatibabu. Ukiwa na pesa basi una sauti na hakuna mtu ambaye atakuhadaa ili ajinufaishe,” akasema Bi Kobia.

Alitoa wito kwa umma kujifahamisha na namna ya kuwatambua wahubiri waongo wenye tamaa ya kuzima kiu chao cha mapenzi kwa wanawake wasiojiweza na akataka wananchi kukemea suala hilo kwa kinywa kipana bila kuogopa.

“Maombi yetu husikizwa moja kwa moja na Mwenyezi Mungu. Dhuluma zinazotekelezewa wanawake zinafaa kuorodheshwa kama za kijinsia. Wanawake wengi wanaopitia dhuluma hizi na hunyamaza na mara nyingi ni wale maskini wasiojiweza,” akaongeza Prof Kobia.

Waziri huyo msomi pia aliwaomba vijana kutotegemea mapeni machache kutoka kwa wanasiasa akiwataka wajiajiri na kutia bidii maishani.

Prof Kobia alisisitiza kwamba Rais Uhuru Kenyatta ana nia ya kuhakikisha vijana, walemavu na wanawake wanajiendeleza kupitia fedha zinazotolewa kupitia vyama vya ushirika.

Naibu Gavana wa Meru Titus Ntuchiu ambaye pia alihudhuria hafla hiyo aliwaomba vijana kutokata tamaa wakikosa ajira za serikali baada ya kumaliza masomo vyuoni.

Mbunge wa Imenti ya Kaskazini Rahim Dawood naye alisema yupo tayari kushirikiana na serikali ya kaunti kusaidia makundi ya vijana, walemavu na akina mama kuanzisha miradi ya kuwanufaisha na kuwapa mapato mazuri.