Habari Mseto

Waziri atetea ajira ya madaktari kutoka Cuba

March 27th, 2018 2 min read

Na CECIL ODONGO

WAZIRI wa Afya Bi Sicily Kariuki amekanusha kwamba madaktari 100 wataalam kutoka Cuba wanaotarajiwa hapa nchini watatoa ushindani na kusababisha ukosefu wa kazi kwa zaidi ya madaktari 1200 ambao hawana ajira.

Kulingana na waziri huyo, madaktari hao, watakaoajiriwa kwa mkataba wa miaka miwili watawapa ujuzi madaktari wa Kenya kuhusu uendeshaji wa sekta ya afya nchini kwao na kupendekeza uboreshaji wake hapa nchini.

“Madaktari hao kando na kutoa huduma spesheli katika hospitali zetu, watakuwa na wajibu wa kuwanoa madaktari wa nyumbani na kuwapa ujuzi wa kuimarisha sekta ya afya hapa kwetu,” akasema waziri huyo.

Alisema kwamba mfumo wa ugatuzi umesaidia kutekeleza mabadiliko na kusaidia kupanuka kwa taasisi zinazotoa huduma za afya karibu na mwananchi.

“Hospitali zetu kuu zina msongamano mkubwa wa wagonjwa kwa hivyo lengo letu kuu ni kugatua huduma hadi zile za mashinani na kuwahamasisha wananchi kuamini huduma zao,” akasisitiza.

Waziri huyo alikuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa warsha ya siku tatu ya afya katika hoteli ya Laico Regency mada kuu ikiwa ni ‘Namna ya kuhakikisha huduma sawa ya afya kwa wote.’

Naibu Gavana wa Isiolo Abdi Ibrahim ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa Kamati ya afya katika Baraza la magavana Dkt Mohamed Kuti alisema kwamba kaunti zinakabiliwa na changamoto ya uchache wa madaktari na kwamba wanalazimika kuajiri wengine kutokana na vipindi vya mafunzo vya kila mara kwa waliokuwepo.

“Kaunti zina madaktari wachache sana, kwa mfano kaunti ya Isiolo asilimia sitini ya madaktari wetu huandaliwa mafunzo na waliosalia huwa wachache wasioweza kutoa huduma bora. Wao huchelewa kazini na kupinga juhudi zetu za kuwafanya wawajibike,” akasema.

Alikariri tamko la waziri la kuhakikisha kwamba msongamano mkubwa wa wagonjwa unaoshuhudiwa katika hospitali kubwa kama Kenyatta na ile ya Moi Eldoret utapungua iwapo serikali itawekeza katika kuiinua hospitali ndogo ndogo za mashinani.

Ilibainika wazi katika warsha hiyo kwamba sekta ya afya ina mianya kupitia taasisi zake dhaifu na ukosefu wa sheria zinazofaa kuhakikisha uwajibikaji.

Khama Rogo, ambaye ni mtaalam wa kiafya anayetambulika barani Afrika na Chansela wa Chuo Kikuu cha Moi Miriam Were walisisitiza kwamba ili nchi iweze kujinadi kuwa sekta hiyo imeimarika lazima wakenya maskini wajumuishwe kwenye mpango wa Bima ya afya.