Habari Mseto

Waziri Eugene asema serikali itajenga mabwawa madogo kwa gharama nafuu

October 24th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

ILIPOCHUKUA hatamu za uongozi mwaka 2013 serikali ya Jubilee iliahidi kufanya miradi mbalimbali ya maendeleo katika kila pembe ya taifa.

Kufikia sasa, mingi ya miradi hiyo ama haijaafikiwa kikamilifu au inakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Miongoni mwayo ni mabwawa.

Miradi hiyo imegubikwa na sio tu sakata za ufisadi na ubadhirifu wa fedha, lakini pia malumbano katika majukwaa ya kisiasa ambapo kidole cha lawama kinanyooshewa ama kwa huyu mwanasiasa au yule.

Vya hivi karibuni ni visa vya miradi ya mabwawa ya Kimwarer na Aror katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Kulingana na asasi za uchunguzi, kuna madai kwamba zaidi ya Sh15 bilioni zimefujwa kupitia mabwawa hayo.

Waziri wa Ugatuzi Euegene Wamalwa alisema Jumanne kwamba serikali inapania kujenga mabwawa madogo; tena kwa gharama nafuu.

Akikiri kuwa mradi wa mabwawa nchini umekumbwa na changamoto tele, waziri huyo alisema hatua hiyo itasaidia kufanikisha malengo ya serikali kwa wananchi.

“Tunalenga kupunguza gharama ya mabwawa yanayochukua zaidi ya miaka mitano kukamilika na kugharimu mabilioni ya pesa, kwa kuchimba mabwawa madogo na ya gharama nafuu,” akasema Waziri Eugene.

Akaongeza: “Tunaelewa changamoto zipo kama vile kashfa ya Kimwarer na Aror, lakini lazima tutafute namna ya kuzitatua.”

Alisema hayo kwenye mahojiano na runinga ya Citizen.

Hata hivyo, waziri alisema baadhi ya miradi kama vile bwawa la Thwake linalojengwa katika mpaka wa Kitui na Makueni na Thiba (Kirinyaga), imefanikiwa. Hata hivyo, makala za ufichuzi ya kampuni ya Nation Media Group kwa ushirikiano na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi ziliangazia jinsi ambavyo maji lengwa ya bwawa hilo yamechafuliwa.

Eugene alisema mabwawa yatakayotengenezwa yatasaidia kukusanya maji hasa msimu wa mvua kubwa na hata iliyopitiliza, hatua aliyoisifia akisema itasaidia kuangazia mafuriko yanayoshuhudiwa maeneo mbalimbali nchini.

“Mabwawa hayo yataweza kuteka maji wakati wa mafuriko. Tunahimiza serikali za kaunti zitekeleze wajibu wao, nasi (serikali kuu) tutimize yetu,” akasema waziri.

Kufuatia mvua kubwa ya mafuriko inayoendelea kunyesha maeneo tofauti nchini, watu 20 wameripotiwa kufa maji. Mvua ya msimu mfupi wa Oktoba – Desemba ya mwaka huu inasemekana kuwa kubwa kuliko ya miaka iliyopita. Tayari Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa, mnamo Jumatano ilitoa tahadhari kufahamisha umma kwamba mvua iliyopitiliza kiwango itaendelea kunyesha kwa kipindi kingine cha mwezi huu Oktoba, Novemba na hata mwanzoni mwa Desemba.

Idara ya utabiri wa hewa imeonya kuwa hali inayoshuhudiwa itaendelea, watu wakihimizwa kuhama kwa muda maeneo hatari kama vile kingo za mito, bahari na yenye milima na mabonde.