HabariSiasa

WAZIRI KIGEUGEU: Atapatapa kuhusu maamuzi ya uchukuzi

January 31st, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

KWA mara nyingine tena, Waziri wa Uchukuzi, Makao na Miundomsingi, James Macharia, amekosa kutimiza tangazo lake baada ya Jumatano jioni kubadilisha kauli kuhusu mpango wa kuondoa magari katikati mwa jiji la Nairobi, siku mbili pekee baada ya kusema hayo.

Mnamo Jumatatu, Bw Macharia alitangaza kuwa kuanzia Februari 1 mwaka huu, magari ya umma na kibinafsi hayangeruhusiwa katika baadhi ya baraara ara za jiji siku za Jumatano na Jumamosi ili kuwapa wachuuzi fursa ya kuuza bidhaa katika barabara hizo.

Utekelezaji wa mpango huo ulitarajiwa kuanza kesho Ijumaa kwa majaribio lakini jana jioni, alituma taarifa kwa vyombo vya habari kutangaza kuwa umesimamishwa.

“Kama mnavyojua, maandalizi ya siku za kutokuwa na magari katikati mwa jiji la Nairobi yanaendelea na majaribio yalipaswa kuanza Februari 1. Hata hivyo, usajili wa wachuuzi kwa njia ya kielektroniki haujakamilika ilivyotarajiwa. Hii ni hatua ya kiusalama ambayo ni lazima ikamilishwe. Kwa hivyo, jaribio hilo limesimamishwa hadi itakapotangazwa tena,” alisema.

Maelezo yake yanazua maswali kuhusu sababu za kutangaza kuanza kwa mpango huo kabla ya masuala aliyotaja kushughulikiwa kwanza.

Hii sio mara ya kwa Waziri Macharia kujikwaa katika matangazo yake kuhusu hatua muhimu zinazochukuliwa na wizara yake.

Mwaka jana, alitangaza kuwa serikali ingeagiza mabasi maalum ya uchukuzi jijini Nairobi maarufu kama BRT kutoka Afrika Kusini kabla ya kubadilisha kauli hiyo na kusema yatatengenezewa nchini.

“Nimemtuma Katibu wa Wizara yangu nchini Afrika Kusini kujadili ununuzi wa mabasi hayo. Kila kitu kikienda sawa, yatawasili nchini kuanzia mwisho wa Juni,” Bw Macharia alisema Mei 25, 2018 akimaanisha yangewasilishwa mwezi uliofuata wa Juni.

Juni ilipofika, Bw Macharia alitangaza kuwa serikali iliamua kununua mabasi hayo nchini badala ya kuyaagiza kutoka Afrika Kusini, alipokuwa akizungumza katika kiwanda kipya cha kampuni ya Kenya Coach Industries (KCI) jijini Nairobi.

“Hatujawahi kupanga kuagiza mabasi ya BRT kutoka nje ya nchi. Tumejitolea kushauriana na watengenezaji wa humu nchini kutuuzia mabasi haya na kuweka sera ambazo zitawapa motisha wawekezaji katika sekta ya magari nchini,” alisema mnamo Juni 21.

MABASI YA MWENDO KASI

Lakini mnamo Jumatatu, Bw Macharia alisema kinyume cha kauli yake ya mwaka jana alipoeleza kuwa mabasi hayo yataletwa nchini kutoka Afrika Kusini.

“Mabasi 64 yatatoka Afrika Kusini kutumika katika majaribio ya mpango huu,” alisema Bw Macharia mnamo Jumatatu wiki hii.

Mwishoni mwa mwaka jana alitangaza msako dhidi ya magari hasa ya matatu, ambao ulianza Novemba kwa vishindo kote nchini na kuendelea kwa wiki mbili kabla ya kufifia na mambo yakarudi hali ya kawaida.

Wiki jana Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) iliyokuwa chini ya Waziri Macharia ilihamishiwa Wizara ya Usalama wa Ndani.

Wakati wa msako huo kulikuwa na uhaba wa magari na Bw Macharia alitangaza kuwa magari ya moshi yanayohudumu jijini Nairobi yangeongezwa kutoka 12 hadi 18, jambo ambalo halikutendeka.

Aidha, alitangaza kuwa mabasi ya Shirika la Vijana wa Huduma kwa Taifa (NYS) yangeongezwa katika barabara za Nairobi ili kusaidia wakazi. Mabasi machache yalihudumu kwa muda mfupi kisha yakaondolewa.

Mnamo Jumanne alitangaza kuwa serikali Machi itaanza kutoza wafanyakazi wa umma na wa kibinafsi asilimia 1.5 ya mshahara wao kufadhili mpango wa makazi nafuu wa serikali.

Alitoa tangazo hilo kukiwa na kesi kortini lakini hakueleza ilivyosuluhishwa na Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) uliowasilisha kesi hiyo haujasema lolote.