Kimataifa

Waziri matatani kwa kukejeli watu wenye njaa

January 28th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

WAZIRI mmoja nchini Uganda, ameshtumiwa vikali baada ya kuwaita watu waliofariki kutokana na njaa nchini humo kuwa “wajinga”.

Watu wengi wametaja matamshi hayo, yaliyotolewa na Waziri Henry Okello Oryem wa Mashauri ya Kigeni kuwa “ya kusikitisha”.

Mnamo 2022, zaidi ya watu 2, 200 walifariki nchini humo kutokana na njaa na maradhi yanayohusiana na ukosefu wa chakula cha kutosha eneo la kaskazini, kulingana na ripoti iliyotolewa na shirika moja la kutetea haki za binadamu.

Hata hivyo, waziri huyo alisema kuwa hakuna mtu yeyote anayefaa kufariki kutokana na njaa nchini humo, kwani taifa hilo lina hali nzuri ya anga na ardhi yenye rutuba.

“Ni mtu mpumbavu, mpumbavu kabisa, anayeweza kufariki kutokana na njaa nchini Uganda,” akasema waziri huyo, kwenye mahojiano na kituo cha televisheni cha NTV Uganda Ijumaa, Ijumaa, Januari 26, 2024.

Akaeleza: “Ukifanya kazi kwa bidii, kuna ardhi nchini Uganda. Hali ya hewa ni nzuri, licha ya mabadiliko ya tabianchi. Ukifanya bidii kwa kuhakikisha umeamka asubuhi na mapema, ulime shamba lako, upande mbegu, udumishe shamba lako, kweli, ni vipi unaweza kukosa chakula?”

Kando na kusababisha vifo vya watu wengi kaskazini mashariki mwa taifa hilo, hali hiyo iliwaacha karibu watu 500, 000 katika hali mbaya ya njaa.

Hilo ni kulingana na ripoti iliyotolewa na Tume ya Haki za Binadamu ya Uganda (UHRC).

Matamshi ya waziri huyo yamezua ukosoaji mkubwa.

Kwenye mitandao ya kijamii, raia wa taifa hilo na mataifa jirani kama Kenya walimlaumu waziri huyo kwa kujitia hamnazo kuhusu yale yanayoendelea nchini mwake kuhusu ukosefu wa chakula.

“Ni sikitiko kubwa waziri kutoa matamshi kama hayo ilhali anafahamu hali ya kiangazi na ukosefu wa chakula ambayo huwa inatokea katika baadhi ya maeneo,” akasema Bi Harriet Anabo, ambaye ni raia wa Uganda kupitia mtandao wa ‘X’ (awali Twitter).

Mwanahabari Charles Onyango-Obbo aliyataja matamshi ya waziri huyo kama “upofu wa kujiwekelea”.

“Anafahamu yale yanayoendelea nchini kutokana na njaa,” akasema.