Kimataifa

Waziri mjamzito asisimua kuendesha baiskeli hadi hospitalini

August 20th, 2018 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

WAZIRI wa Masuala ya Wanawake nchini New Zealand Julie Anne Genter Jumapili alishangaza ulimwengu baada ya kuendesha baiskeli hadi hospitalini, akiwa mjamzito.

Bi Genter aliamua kuendesha baiskeli kwa umbali wa kilomita moja kutoka nyumbani kwake hadi hospitali ya jiji la Auckland kupata huduma za ujauzito wa mwanawe wa kwanza, tukio lililowaacha wengi wakishangaa.

Akizungumza baada ya tukio hilo, waziri huyo alisema pamoja na mumewe waliamua kutumia baiskeli kufika hospitalini kwani gari halikuwa na nafasi ya kutosha.

“Mume wangu name tuliamua kuendesha baiskeli kwani gari halikuwa na nafasi ya kutosha hadi wafanyakazi, lakini pia hiyo inaniweka katika hali nzuri sana,” akachapisha mtandaoni.

Aidha, aliweka picha yake akiwa na baiskeli, wakati huu akiwa na uja uzito wa wiki 42. Bi Genter amekuwa shabiki mkuu wa uendeshaji wa baiskeli na hatua yake hiyo ilikuwa mojawapo tu ya kampeni za kupigia debe mazoezi hayo.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 38 alifurahia safari hiyo ambayo alisema sana ilihusisha miteremko, akisema angejua angekuwa amefanya hivyo mara nyingi mbeleni ili ufikapo wakati wa kujifungua asiwe na ugumu.

“Naona hata ningeendesha hata zaidi wiki chache zilizopita ili kurahisisha kazi,” akachapisha waziri huyo.

Tukio lake hilo limekuja wiki chache baada ya waziri mkuu wan chi hiyoJacinda Ardern kujifungua na kurejea bungeni.

Bi Ardern alijifungua katika hospitali hiyo ya Auckland ambayo ni ya umma na ambapo Bi Genter aidha anatarajia kujifungulia.