Waziri Mkuu asema hatahudhuria  mazishi ya mume wa Malkia Elizabeth

Waziri Mkuu asema hatahudhuria mazishi ya mume wa Malkia Elizabeth

Na MASHIRIKA

WAZIRI Mkuu wa Uingereza, Borris Johnson, hatahudhuria mazishi ya Mwanamfalme Philip, Jumamosi ijayo, imesema afisi yake kwenye taarifa.Msemaji katika afisi hiyo alisema uamuzi huo uliafikiwa ili kuzingatia kanuni za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Taarifa kutoka familia ya kifalme zilisema ni watu 30 pekee watakaoruhusiwa kuhudhuria mazishi hayo, yatakayofanyika katika makao ya kifalme ya Windsor Castle.Ripoti zilisema Johnson alifanya uamuzi huo ili “kutochukua nafasi ambayo ingetengewa jamaa za mwanamfalme huyo.”

“Kutokana na masharti ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona, ni watu 30 pekee watakaoruhusiwa kuhudhuria mazishi ya Mwanamfalme Philip,” akaeleza msemaji huyo.

“Waziri Mkuu atazingatia na kuheshimu matakwa yote ya familia ya kifalme. Ili kuwaruhusu jamaa wengi kushiriki katika hafla hiyo, hatahudhuria mazishi hayo Jumamosi,” akaeleza.

Kama ishara ya kuonyesha hekima kwa mwanamfalme huyo, kampeni za mabaraza ya miji na mabunge ya Scotland na Wales zimesimamishwa kwa muda.Chaguzi hizo zimepangiwa kufanyika Mei 6.

Bunge la Kitaifa na mabunge ya majimbo katika maeneo ya Cardiff na Edinburg yataandaa vikao maalum leo, kuwaruhusu wabunge kutuma rambirambi zao kwa marehemu.

Mwanamfalme huyo alikuwa mumewe Malkia Elizabeth na wamekuwa kwenye ndoa kwa zaidi ya miaka 70.Marehemu alifariki Ijumaa akiwa na umri wa miaka 99.Katika mazishi hayo, hakutakuwa na misafara ya kumwomboleza, kama ilivyo kawaida kwa mazishi ya jamaa wa familia ya kifalme.

“Hafla hiyo itatumika kusherehekea na kutambua mchango wa marehemu kwa Malkia, Uingereza na nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola,” akaeleza msemaji wa kifalme.

Kabla ya mazishi hayo kuanza, raia wote nchini humo watanyamaza kwa dakika moja kukumbuka maisha yake.Licha ya habari kuibuka kwamba waziri mkuu hatakuwepo, ingali kubainika wale watakaohudhuria.

Hata hivyo, miongoni mwa wale watakaokuwepo ni Mwanamfalme Harry, aliyezua msisimko katika familia hiyo baada ya kufanyiwa mahojiano na mtangazaji Oprah Winfrey, nchini Amerika pamoja na mkewe, Meghan, mwezi uliopita.

Ripoti zilisema Meghan hatahudhuria kutokana na ushauri wa daktari wake kwani ni mjamzito.Washiriki wote watazingatia kanuni za kudhibiti corona, ambazo ni kuvaa barakoa, kutokaribiana na kuosha mikono yao.

Kufuatia kifo chake, viongozi mbalimbali duniani walituma jumbe za rambirambi, wakimwomboleza kama “nguzo kuu” iliyompa nguvu Malkia Elizabeth kuliongoza taifa hilo.Vikosi vya usalama nchini humo vilimwomboleza Jumamosi kwa kufyatua risasi hewani katika miji ya London, Edinburg, Cardiff, Belfast na Gibraltar.

You can share this post!

LEONARD ONYANGO: Ukweli ni kuwa Kenya yahitaji suluhu ya...

China kuchanganya chanjo mbalimbali kukabili corona