Kimataifa

Waziri Mkuu na mawaziri wote wa Urusi wajiuzulu

January 15th, 2020 1 min read

CHARLES WASONGA na MASHIRIKA

MOSCOW, Urusi

SERIKALI zima la Urusi Jumatano imejiuzulu baada ya Rais Vladimir Putin kupendekeza mapendekezo kadhaa kwenye katiba ya nchi hiyo.

Waziri Mkuu Dmitry Medvedevpamoja na mawaziri wote wamejiondoa mamlakanni kwa kile wamesema ni nia ya Bw Putin kupunguza mamlaka ya mrithi wake.

Kwenye hotuba yake ya kila mwaka kwa bunge, Putin alipendekeza kufanyike kura ya maamuzi kufanyia marekebisho katiba ili kuongeza mamlaka ya bunge la nchi- japo mfumo wa uongozi wa bunge bado utadumishwa.

“Naona ni bora wananchi wapige kura kuamua kuhusu marekebisho yote ya katiba yaliyopendekezwa,” Putin akasema bila kutaja tarehe ambapo kura hiyo ya maamuzi itafanyika.

Dmitry Medvedev ambaye aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Putin atateuliwa kuwa naibu Mkuu wa Baraza la Usalama la Urusi, chini ya mabadiliko hayo.

“Hii inaonyesha kuwa Putin anamwamini Medvedev, ambaye amekuwa mwandani wake kwa miaka mingi,” akasema Aleksandra Godfroid, mwanahabari anayehudumu jijini Moscow.

Kauli ya Putin wakati wa hotuba hiyo, inajiri wakati ambapo wachanganuzi wanafuatilia kwa makini kuona jinsi anatafanya mabadiliko katika siasa za nchi hiyo kabla ya mwaka wa 2024 wakati muhula wake wa uongozi utafikia tamati.

Katiba inamhitaji kuondoka mamlakani wakati huo ambapo atakuwa ametimu umri wa miaka 71.

Katika mabadiliko ya Katiba yanayoungwa mkono na Putin, mamlaka ya bunge yataongezwa ambapo wabunge watakuwa na uwezo wa kuchagua waziri mkuu na mawaziri.

Alipokuwa akijiuzulu Medvedev alisema kwamba, kufuatia mabadiliko ambayo yatafanyika katika Katiba, anahisi rais “anapasa kupewa nafasi aendeleze mabadiliko na kupendekeza aina ya serikali anayopenda.”

Chini ya mabadiliko yanayopendekezwa kufanyiwa Katiba, kimsingi serikali itateuliwa na bunge, tofauti na hali ilivyo sasa.

Hata hivyo, Rais atakuwa na mamlaka ya kuifuta kazi serikali endapo hataridhika na utendakazi wake.

Rais pia atasimamia wanajeshi, polisi na maafisa wengine wa usalama, kando na kuteua maafisa wa kusimamia asasi hizo.