Waziri Namwamba atoa onyo kali baada ya Kenya kuondolewa marufuku

Waziri Namwamba atoa onyo kali baada ya Kenya kuondolewa marufuku

NA JOHN ASHIHUNDU

WAZIRI wa Michezo, Ababu Namwamba ameonya kwamba kuondolewa kwa marufuku na Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) dhidi ya Kenya hakutatumika kuendeleza ufisadi katika Shirikisho la Soka Nchini (FKF).

Akihutubia waandishi jijini Nairobi, Namwamba alisema, japo FIFA imechukua hatua hiyo, kesi ya ufisadi inayomhusisha rais wa FKF, Nick Mwendwa itaendelea na hukumu kutolewa kulingana na sheria.

Uamuzi wa FIFA umejiri siku chache tu baada ya Namwamba kukutana na rais wa shirikisho hilo, Gianni Infantino nchini Qatar walipokutana kushuhudia mechi za fainali za Kombe la Dunia.

Kenya ilipigwa marufuku kutojihusisha katika masuala yeyote ya soka, baada ya Serikali kuvunjilia mbali shirikisho la FKF mwaka uliopita na kuteua kamati mpito ikiongozwa na Jaji mstaafu Aaron Ringera kusimamia mchezo huo nchini.

Marufuku hiyo ilizuia timu za Kenya kucheza katika mashindano yoyote ya kimataifa, ama hata marefari wake kusimamia mechi zozote za kimataifa. Kadhalika marufuku hiyo ilizima kabisa wachezaji wa Kenya kujiunga na klabu za ng’ambo.

Marufuku hayo yalipotangazwa, timu za taifa ikiwemo Harambee Starlets ziliondolewa kwenye mashindano ya kimataifa, lakini baada ya marufuku hiyo kuondolewa, wanasoka wa Kenya watapata fursa nyingine ya kuendeleza vipaji vyao kimataifa.

“Nitakutana na viongozi wa FKF kujadili hali ya baadaye ya Kenya kusonga mbele katika maswala ya soka, baada ya kukaa nje kwa miezi kadhaa,” alisema Namwamba.

Wakati huo, Starlets ilikuwa kambini ikijiandaa kucheza na Crested Cranes ya Uganda ugenini na hapa nyumbani katika mchujo wa kuwania nafasi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika kwa timu za wanawake.

Uamuzi huo ulipoidhinishwa mwishoni mwa mwezi Machi, wanachama 198 wa FIFA walipiga kura ya kuunga mkono, huku mwanachama mmoja tu akipiga kura ya kupinga.

Mbali na vikwazo hivyo, Kenya haikupata ufadhili wowote kutoka kwa shirikisho hilo la kandanda duniani, hadi mahitaji muhimu yatimizwe, yakiwemo kurejeshwa kwa mamlaka ya kuendesha shughuli za soka kwa kamati utendaji na katibu mkuu.

Masaibu ya Kenya yalianza tarehe 11, mwezi Novemba 2021 baada ya aliyekuwa Waziri wa Michezo, Amina Mohamed kuvunjilia mbali kamati ya FKF na kuteua kamati ya mpito kusimamia kandanda kwa kipindi kifupi.

Waziri alichukua hatua hiyo baada ya rais wa FKF, Nick Mwendwa kutajwa kwenye ghashfa ya matumizi mabaya ya fedha za umma, na kutiwa mbarani na kushtakiwa kwa makosa manne ya ufisadi.

Lakini kwenye barua iliyotoka makao makuu ya FIFA, jana Jumatatu, Kenya imeondolewa marufuku hiyo baada ya Serikali kurejesha uongozi wa FKF na kuvunjilia mbali kamati ya mpito iliyoteuliwa.

Kwenye barua hiyo iliyowekwa saini na Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Fatma Samoura, FIFA ilisema haiingilii uchunguzi dhidi ya Mwendwa, wala haiungwi mkono vitendo vya ufisadi.

“Tungependa kuwafahamisha kwamba baada ya kupokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa FKF, Barry Otieno kuthibitisha hatua ya Waziri Ababu Namwamba kurejesha usukani kamati ya FKF, kamati yetu ilikutana mnamo Novemba 25, 2022 na kuamua kuondoa marufuku iliyowekewa Kenya.”

“Kutokana na uamuzi wetu, sasa FKF iko huru kusimamia masuala ya soka nchini Kenya, lakini kamwe hatuingilii shughuli za kesi inayo Kortini dhidi ya shirikisho hilo.”
  • Tags

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Cameroon wafunganya virago Qatar...

Firat akaribia kurejea kushika usukani Kenya

T L