Michezo

Wazito, Kisumu All Stars na Nairobi Stima zafukuzana jedwalini

May 21st, 2019 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

Huku zikiwa zimebakia mechi tatu msimu wa Supa Ligi kukamilika nchini, timu za Wazito FC, Kisumu All Stars na Nairobi Stima zinaendelea kubakia katika mdwara wa kuwania nafasi mbili za kufuzu kwa ligi kuu ya SportPesa msimu ujao.

Hii ni baada ya timu hizo kuandikisha ushindi katika mechi zao zilizochezwa mwishoni mwa wiki katika viwanja mbali mbali.

Katika mechi hizo, Wazito waliibuka na ushindi mkubwa wa 6-0 dhidi ya Green Commandos ambao wanakabiliwa na hatari ya kushuka daraja.

Kutokana na ushindi huo, Wazito wanaongoza msimamo wa ligi hiyo kwa pointi 69, moja mbele ya Kisumu All Stars wanaokamata nafasi ya pili baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Coast Stima katika mechi iliyochezewa Moi Stadium, Kisumu.

Mjini Naivasha, wenyeji Nairobi Stima ambao wamefikisha pointi 67 walipata ushindi mwempamba wa 3-2 dhidi ya Kangemi All Stars katika mechi iliyochezewa ugani Karuturi. Vijana hao wa kocha George Owoko, wako mbele ya Ushuru kwa tofauti ya pointi nne.

Matokeo ya mechi ya Naivasha yameiacha Kangemi katika nafasi ya mwisho jedwalini baada ya kufikisha pointi 22.

Kwingineko, Shabana waliandikisha ushindi wa 3-1 dhidi ya Fortune Sacco kwenye mechi iliyochezewa Gusii Stadium na kupanda kutoka nafasi ya 10 hadi ya nane.

Vijana hao wanaonolewa na Gilbert Selebwa wameahidi kucheza kwa bidi mechi zilizobakia, huku wakilenga kumalizz msimu katika nafasi nzuri.

Matokeo ya mechi kwa ufupi:

Kisumu All Stars 1 Coast Stima 0; Ushuru 2 St Joseph Youth 1; Bidco United 3 Modern Coast Rangers 0; Wazito 6 Green Commandos 0; Administration Police 0 Migori Youth 0; Shabana 3 Fortune Sacco 1; Nairobi Stima 3 Kangemi All Stars 2; Eldoret Youth 0 Kenya Police 2; Thika United 1 Kibera Black Stars 2; FC Talanta 1 Nairobi City Stars 1.