Michezo

Wazito wampokeza Fred Ambani mikoba ya ukufunzi

August 11th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

WAZITO FC wamempokeza Fred Ambani mikoba yao ya ukufunzi na kumteua beki wa zamani wa Harambee Stars, Salim Babu kuwa kocha msaidizi.

Katika taarifa yao, Wazito FC wamethibitisha kwamba Ambani kwa sasa anachukuwa iliyokuwa nafasi ya Mwingereza Stewart Hall aliyewahi pia kudhibiti mikoba ya mabingwa mara 13 wa Ligi Kuu ya Kenya, AFC Leopards.

Itakuwa mara ya pili kwa Ambani kuwatia makali mabwanyenye wa Wazito FC baada ya kuongoza kikosi hicho kupanda ngazi kutoka Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL) katika msimu wa mwishoni mwa msimu wa 2018-19.

“Nashukuru usimamizi wa klabu kwa kuniamini kwa mara nyingie. Wazito ni kikosi ninachokistahi sana. Lengo langu kwa sasa ni kufanya kazi na kila mmoja kambini na kuyafikia malengo ya kikosi,” akasema Ambani ambaye ni mwanasoka wa zamani wa timu ya taifa ya Harambee Stars.

“Hall ni kocha ambaye nilifanya naye kazi nyingi kwa ushirikiano. Alinielekeza ipasavyo. Ni nadra sana kupata wakufunzi wa sampuli yake. Namshukuru sana kwa yote aliyonifunza na namtakia kila la heri kokote aendako kwa kuwa najua ubora wa rekodi yake katika ukufunzi utampa nafasi katika kikosi chochote duniani humu karibuni,” akaongeza Ambani.

Babu anajiunga na Wazito baada ya kukatiza uhusiano wake na Western Stima alikokuwa kocha mkuu.

Babu alianza ukufunzi wake katika kikosi cha mabingwa wa KPL 2006, SoNy Sugar akiwa kocha msaidizi pindi baada ya kustaafu soka. Alikwezwa baadaye kuwa mkufunzi mkuu wa kikosi hicho kabla ya kuyoyomea Migori Youth kisha Stima.

Katika kampeni za KPL msimu wa 2018-19, alitawazwa Kocha Bora wa Mwezi mara mbili huku Steven Polack wa Gor Mahia akitwaa tuzo hiyo mara tatu.

“Kujiunga na Wazito ni fursa kubwa katika kukuza maazimio yangu. Kazi yangu ni kuwa kocha msaidizi na kusadia kocha mkuu,” akasema.

“Ambani amekuwa rafiki yangu kwa muda mrefu na tuliwahi kucheza pamoja katika timu ya taifa. Aliponiuliza kuhusu uwezekano wa kujiunga naye, ilikuwa rahisi sana kufanya maamuzi kwa kuwa ni mtu ninayemfahamu vyema na ninaamini kwa pamoja, tutambisha Wazito katika kampeni zijazo,” akaongeza Babu.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu Mtendaji wa Wazito Dennis Gicheru alisema: “Tunawapongeza wakufunzi hawa kwa uteuzi wao. Ambani anaielewa vizuri klabu ya Wazito. Tulimpa mamlaka yote ya kujiteulia msaidizi wake na akamchagua Babu ambaye kwa maoni yetu, pia ni mkufunzi aliye na tajriba ya kipindi kirefu katika ulingo wa soka na rekodi yake inajisema mengi.”