Michezo

Wazito warejea kileleni, Ushuru yateleza

April 22nd, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

USHURU FC ilikosa ujanja na kulazimishwa kujiongezea alama moja kwenye kampeni za kupigania taji la Supa Ligi ya Taifa (NSL), huku Wazito FC ikibeba magoli 4-0 mbele ya Kisumu Allstars na kurejea kileleni mwa kipute hicho.

Wazito FC iliteremka dimbani ikipania kulipiza kisasi baada ya kudungwa mabao 2-0 na Eldoret Youth wiki iliyopita.

Wachezaji hao walionyesha soka safi na kutwaa alama zote tatu walipowazidi nguvu wenyeji wao kwenye mechi iliyopigiwa Moi Stadium, mjini Kisumu.

Wazito iliandikisha mafanikio hayo kupitia Musa Masika aliyepiga makombora mawili safi huku Paul Acguah na Teddy Osok kila mmoja akifanikiwa kucheka na nyavu mara moja.

Nayo Ushuru ambayo hutiwa makali na Ken Kenyatta iliachia alama mbili muhimu ilipokubali kutoka sare ya bao 1-1 na Eldoret Youth ugani Eldoret Show Ground.

Kikosi cha Fortune Sacco kabla ya kushuka dimbani kukabili Nairobi City Stars kwenye mchezo wa Supa Ligi ya Taifa (NSL) uwanjani Camp Toyoyo Jericho, Nairobi. Mechi iliisha sare ya mabao 4-4.

Vilevile wachana nyavu wa Nairobi Stima walitoka nguvu sawa bao 1-1 na Maafande wa Administration Police (AP) na kutinga kati ya tatu bora kwa alama 56, moja mbele ya Kisumu Allstars.

Kutokana na matokeo hayo, Wazito FC inaongoza kwa kukusanya alama 58, mbili mbele ya Ushuru FC baada ya kusakata mechi 28 kila moja. Mechi nyingine, Kangemi Allstars ilizimwa kwa bao 1-0 na Kenya Police.

MATOKEO YA MECHI HIZO

Eldoret Youth 1-1 Ushuru FC

Nairobi Stima 1-1 Administration Police

FC Talanta 1-0 Thika United

Nairobi City Stars 4-4 Fortune Sacco

Kangemi Allstars 0-1 Kenya Police

Modern Coast Rangers 1-1 Migori Youth

Coast Stima 1-1 Kibera Black Stars

Kisumu Allstars 0-4 Wazito FC