Michezo

Wazito wasisitiza watasalia ligini

July 30th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

KOCHA msaidizi wa Wazito FC Ahmed Mohammed amesisitiza kwamba timu hiyo itaepuka shoka la kushushwa daraja japo wanaburura mkia kwenye msimamo wa jedwali la ligi KPL zikiwa zimesalia mechi 10 ligi ifike ukingoni.

Wazito walipoteza 2-3 dhidi ya Posta Rangers katika mechi iliyochezwa  Jumapili 29 uwanjani Camp Toyoyo jijini Nairobi.

Ingawa hali ilikuwa hivyo, Bw Ahmed  amedai kwamba ilikuwa bahati mbaya hawakushinda mechi hiyo na kujukusanyia pointi zote tatu.

“Tulikuwa bora kuwaliko na ilikuwa bahati mbaya tulipoteza . Wanasoka wangu walitia bidii, walidhihirisha ukakamavu na ujasiri mkubwa. Posta wana uzoefu lakini tuliwatoa kijasho kabla ushindi huo kutuponyoka,” akasema Ahmed baada ya mechi hiyo.

Klabu hiyo ipo katika nafasi ya 20 baada ya kupata alama 19 wakiwa wamejibwaga uwanjani mara 24 japo Ahmed amesema ana uhakika watasalia ligini.

“Tupo katika nafasi mbaya lakini nina hakika tutasalia ligini. Hapo awali tulikuwa na matatizo katika safu ya ushambulizi, sasa tuko sawa na lililosalia ni kuimarisha difensi yetu halafu tutaafikia lengo letu la kubakia ligini,” akaongeza Ahmed.

Wazito watatifua vumbi dhidi ya Nzoia Sugar ugani Sudi Kaunti ya Bungoma, Jumapili Agosti 5 katika mechi ya KPL.