Wazozana kuhusu ufanikishaji miradi

Wazozana kuhusu ufanikishaji miradi

 

Na MAUREEN ONGALA

VIONGOZI wa kisiasa katika Kaunti ya Kilifi wameanza kuzozana kuhusu ni nani alishawishi serikali kufanikisha miradi ya maendeleo, huku wakijiandaa kushiriki uchaguzi ujao.

Baadhi ya miradi ambayo utekelezaji wao unazozaniwa ni ule wa kukarabati mifereji ya Baricho-Malindi-Mombasa ili kuboresha usambazaji maji kwa wakazi wa Kaunti za Mombasa na Kilifi.

Miradi mingine ni ya ujenzi wa barabara ambapo kufikia sasa barabara nyingi zimefanyiwa ukarabati kama vile barabara kuu ya Kaloleni-Mavueni.

Wanasiasa wa kaunti hiyo ambayo ilikuwa na ufuasi mkubwa wa ODM katika uchaguzi uliopita, sasa wanatumia miradi hiyo kama chambo cha kisiasa wanapojiandaa kuwania viti mbalimbali mwaka ujao.

Viongozi hao huegemea mirengo ya Rais Uhuru Kenyatta, naibu wake William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga.Hivi majuzi wakati Dkt Ruto alipozuru Kilifi, Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya alimmiminia sifa tele kwa “kutimiza ombi lake” la kutia lami barabara ya Kibaoni-Ganze-Bamba.

Hii ilikuwa ni baada ya Dkt Ruto kutangaza kuwa shughuli ya kutoa kandarasi kwa ujenzi huo ilikamilika.

“Nimeona matunda ya kuwa rafiki wa karibu wa naibu rais. Nilienda kwake nikamwomba anipigie lami barabara inayotoka Kibaoni katika Chuo Kikuu cha Pwani hadi Ganze akaagiza Mamlaka ya Barabara za Mashambani (KERRA) ijenge barabara hiyo,” akasema.

Hata hivyo, Mbunge wa Ganze, Bw Teddy Mwambire alipuuzilia mbali madai hayo na kusema Rais Kenyatta ndiye alikuwa ameahidi kukamilisha barabara hiyo alipozuru Kilifi mwaka uliopita.

Bw Mwambire ambaye ni mwanachama wa ODM alidai kuwa, yeye ndiye alimwomba Bw Odinga amhimize rais barabara hiyo ijengwe.

Kando na wawili hao, Waziri Msaidizi wa Ugatuzi, Bw Gideon Mung’aro na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Bw Dan Kazungu pia wamekuwa wakibishana kuhusu miradi ya maendeleo hasa katika maeneo ya Malindi na Magarini.

Wawili hao ambao wamepanga kuwania ugavana mwaka ujao wakati kipindi cha pili cha Gavana Amason Kingi kitakapokamilika, wanaaminika kumezea mate tikiti ya ODM.Bw Kazungu aliwahi kuwa mbunge wa Malindi naye Bw Mung’aro alikuwa mbunge wa Magarini.

Wiki iliyopita, Bw Mung’aro alidai kuwa yeye ndiye alishinikiza serikali kujenga barabara ya Malindi-Sala Gate na daraja la Baricho.

Alisema pia ni kwa ushawishi wake ambapo miradi mingi mingine ilifanikishwa kama vile barabara ya Mariakani-Bamba na Sabaki-Marafa.

Hata hivyo, Bw Kazungu alisema yeye ndiye aliwasilisha ombi bungeni alipokuwa mbunge ili barabara ya Malindi-Sala Gate ijengwe.

Alizidi kusema kuwa, wakati alipoandamana na Rais Kenyatta kwa ziara katika mataifa ya Uganda na Ethiopia alipata nafasi nzuri ya kumweleza kuhusu miradi inayohitajika kutekelezwa Kilifi ndipo rais akaahidi serikali yake ingeingilia kati.

You can share this post!

Kamishna aagiza wauzaji wa barakoa feki wanaswe

Muturi awekewa presha aungane na Ruto, si Raila