Habari

Wazozania jina la Uhuru

October 28th, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO na COLLINS OMULO

NAIBU Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga walitumia jina la Rais Uhuru Kenyatta kuwashawishi wakazi wa Kibra kuwapigia kura wawaniaji wa vyama vyao kwenye uchaguzi mdogo unaotarajiwa Novemba 2019.

Kila mmoja wa wawili hao alieleza uhusiano wake wa karibu na Rais Kenyatta kama utakaosaidia kupeleka maendeleo Kibra iwapo wawaniaji wa pande zao watashinda.

“Hao wengine wakileta pesa chukueni lakini kura mpigie Imran Okoth. Ikiwa humpendi Imran, pigia Baba kura. Acha Imran ashikilie hapa Kibra na mimi nishikilie huko Ikulu,” akasema Bw Odinga akihutubia mkutano wa kampeni Jumapili mtaani Kibra.

Uhusiano mwema wa Bw Odinga na Rais Kenyatta tangu mwaka 2018 umefanya serikali kupeleka maendeleo zaidi katika maeneo yanayotambuliwa kuwa ngome za upinzani hasa Nyanza.

Dkt Ruto naye aliwasili mtaani Kibra jioni ambapo alisema kuwa mwaniaji wa chama cha Jubilee, McDonald Mariga ndiye mwenye uwezo wa kuleta mabadiliko katika mtaa huo kwa sababu ni wa chama cha Rais Kenyatta.

“Watu wa Kibra wamechoka kudanganywa. Eneobunge hili limekuwa na sifa ya umaskini na ni Bw Mariga tu ambaye ataleta mabadiliko akifanya kazi na Rais. Kibra haitawahi tena kuwa kitovu cha vita, nyumba za mabanda na umasikini,” akasema Dkt Ruto.

Uchaguzi huo wa Kibra ni muhimu kwa Dkt Ruto na Bw Odinga kwani wanautumia kupima uwezo wao kisiasa kufuatia tofauti zao kubwa.

Bw Odinga anajitahidi kuhakikisha umaarufu wake uko dhabiti katika eneo hilo huku Dkt Ruto akikazana kuonyesha kuwa anaweza kukomesha umaarufu wa kiongozi huyo wa ODM katika Kibra.

Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alisisitiza kuwa Kibra ingali ngome kuu ya Bw Odinga hivyo Bw Okoth ana nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi mdogo wa ubunge utakaofanyika Novemba 7.

“Kuna watu wanauliza kwa nini chama cha ODM kinafanya kampeni katika ‘nyumba ya Baba’. Kwani nyumba ikivamiwa na kunguni huwezi kuinyunyizia dawa kuua wadudu hao? Tunachofanya hapa ni kuua kunguni ambao wamevamia nyumba ya Baba,” akasema Bw Sifuna.

Kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya, Bw Moses Wetang’ula pia waliandaa mikutano ya hadhara na kupinga dhana kwamba Kibra ni ngome ya Bw Odinga.

ODM ilijipata pabaya katika ndimi za vyama vingine vikuu vilivyofanya kampeni jana eneo hilo.

Chama cha ANC kiliwashutumu wafuasi wa ODM baada ya gari la Bw Mudavadi kushambuliwa kwa mawe katika uwanja wa Kamukunji na kukatiza mkutano wa hadhara kumpigia debe Bw Eliud Owalo.

Mawe

Msafara wa ANC ulikuwa ukielekea katika uwanja wa Kamukunji wakati gari lao lilimiminiwa mawe na vijana wasiojulikana.

Chama cha Ford-Kenya pia kiliwashutumu wafuasi wa ODM kwa kutaka kuwapokonya uwanja wa Bukhungu.

Chama cha Ford Kenya kilidai kuwa kilikuwa kimechukua uwanja huo kwa ajili ya mkutano wa mwaniaji wake Khamisi Butichi lakini vijana wa ODM wakajaribu kuwazuia.

Kiti hicho cha Kibra kiliachwa wazi kufuatia kifo cha Ken Okoth mnamo Julai 2019.

Kwingineko, wabunge wapatao 10 wa Jubilee waliapa kupinga BBI iwapo itapendekeza kubuniwa kwa vyeo zaidi serikalini.

Viongozi hao waliokuwa kwenye msafara wa Dkt Ruto katika eneo la Mathira, Kaunti ya Nyeri walisema BBI inashinikizwa kwa wananchi na viongozi.

Walieleza kuwa uanachama wa BBI unapendelea ODM kwani wengi wao ni wanasheria huku wale wa Jubilee wakiwa ni wataalamu wa amani na utangamano.

Kati ya wabunge waliohutubu ni Rigathi Gachagua (Mathira), John Muchiri (Manyatta), Jane Kihara (Naivasha), Kimani Ngunjiri (Bahati), Gichuki Mwangi (Tetu) na Rehema Jaldesa (Isiolo).

Wengine walikuwa Mugambi Rindikiri (Buuri), Halima Mucheke (Kuteuliwa), Aisha Jumwa (Malindi), Rahab Mukami (Nyeri) na Gichuki Mugambi (Othaya).