HUKU USWAHILINI: Wema kupitiliza utapikiwa majungu

HUKU USWAHILINI: Wema kupitiliza utapikiwa majungu

Na SIZARINA HAMISI

HUKU Uswahilini, wengi wetu tunaishi nyumba za kupanga.

Kwamba katika nyumba moja tumeshazoea kuishi familia zaidi ya mbili, ingawa wakati mwingine tunatamani kuishi katika nyumba zetu wenyewe.

Na kawaida kwenye wengi kuna mengi, ili uweze kuishi kwa utulivu na amani kuna jinsi nyingi za kujifunza kuweza kuishi na watu maeneo haya ya kwetu.

Katika kujifunza huku, huna budi kutenda yote kwa kadiri, usiwe mwema sana kupitiliza lakini pia usiwe na roho mbaya iliyopita kiasi.

Binadamu wakati mwingine hawana wema. Pamoja na juhudi zangu za kuwafikia majirani zangu, yaonekana wameanza kuniona najipendekeza kwao na sasa wameamua kunionyesha kwamba wao ni alwatani katika hii mitaa.

Kawaida mie sio mtu wa vurumai, lakini juzi wakati natoka kazini ilibidi nichukue hatua kujinusuru moyo wangu.

Habari za ukarimu wangu kwa watu wachache majirani zetu kwamba niliwatayarishia mapochopocho, ziliwafikia wadaku wa mtaa na wao wakazifikisha kijiweni ambako watoto wa kihuni huweka makazi yao.

Na ndio maana juzi nilidakwa na mnafiki wa mtaa na akanihoji kwa nini nafanya sherehe kwa upendeleo.

Nikataka kujua hizi habari za sherehe za upendeleo amezipata wapi?

Ndipo akasema amesikia habari kwamba nilichagua wale watu maarufu mtaani na nikaacha wale ambao ni wazoefu na walioishi miaka mingi sehemu hizi.

Nikamkumbusha kwamba ukarimu ni hiari na wala sio lazima.

Wakati anayasema haya alikuwa ananikaribia huku akitikiza kifua na kuonyesha ishara ya kunivamia.

Sababu sipendi vita, nikaamua nijiondoe taratibu. Lakini huyu jamaa akanifuata na kuanza kunisukuma.

Mara ya kwanza niliweka kujizuia, mara ya pili nikajipata chini.

Nilipoinuka, sikutaka tena kungojea nikapiga mayowe ya kuomba usaidizi.

Jirani yangu muuza makaa ambaye alikuwa anapita akasikia na kuja haraka na kunikuta nikiinuka huku najikung’uta mavumbi yaliyozagaa mwilini.

“Kulikoni jirani,” akahoji.

Nikamsimulia yaliyotokea ndipo akaniambia tufuatane twende kwake. Huko kwake, ambako anaishi na mkewe aliyeonekana kuniangalia kwa maswali nikajitambulisha na kumweleza yule dada yaliyonikuta.

Akanidakia, “Mimi nakujua sana, tena unavyopenda kujipendekeza kwa watu wengi hapa mtaani. Unadhani hatukujui?”

Kilichonishangaza ni kwamba wema wangu umekuwa ukionekana kama kujipendekeza, wakati madhumuni yangu yalikuwa nia njema!

Nikaelewa kwamba pamoja na mengi mazuri yanayofanywa ni vyema pia kuweka kiasi fulani cha roho mbaya. Sitatenda mabaya, lakini pia nitatenda mema kwa kipimo.

sizarinah@gmail.com

You can share this post!

Wanafunzi 302 ndani kwa uchomaji shule

MAPISHI KIKWETU: Miguu ya kuku chakula kitamu sana

T L