Wembe ‘ule ule’ ndio uliomnyoa Kang’ata

Wembe ‘ule ule’ ndio uliomnyoa Kang’ata

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Murang’a Irungu Kang’ata ameng’olewa kwa njia ambayo analalamika ni potovu, ilhali si tofauti na ile aliyoshabikia ilipotumiwa kumtimua mtangulizi wake Susan Kihika na aliyekuwa kiongozi wa wengi Kipchumba Murkomen.

Dkt Kang’ata alipotimuliwa katika wadhifa wake kama kiranja wa wengi katika seneti kufuatia mkutano maseneta wa Jubilee uliofanyika katika ukumbi wa KICC, Nairobi mnamo Jumanne, alisisitiza hakutendewa haki.

Lakini aliongeza kuwa angeheshimu tu uamuzi huo ikiwa utaungwa mkono na thuluthi mbili ya idadi jumla ya maseneta wa Jubilee kwa “sababu mimi ni kiongozi anayeheshimu sheria.”

“Naamini kuwa ningali kiranja wa wengi katika seneti kwa sababu uamuzi wa kunitimua uliungwa mkono na maseneta 15 pekee kati ya maseneta 25 waliohudhuria mkutano wa leo (jana Jumatano). Maseneta wote waliopewa nafasi ya kuzungumza katika mkutano walipinga kuondolewa kwangu kwa sababu hatua hiyo haikuhimiliwa na makosa mahsusi,” Dkt Kang’ata akawaambia wanahabari nje la jumba la KICC, Nairobi.

Alikuwa ameandamana na maseneta tisa wa mrengo wa Tangatanga wakiongozwa na Kipchumba Murkomen (seneta wa Elgeyo Marakwet) ambao waliondoka kwa hasira kabla ya mkutano huo kuisha wakipinga hatua hiyo.

Spika wa Seneti, Bw Ken Lusaka aliyepokea arafa ya Jubilee kuhusu uamuzi huo Jumanne, Jumatano alithibitisha kwamba chama kilifuata kanuni zote za kisheria.

Kwa msingi huo, Seneta wa Kiambu, Bw Kimani Wamatangi, alitangazwa rasmi kuchukua nafasi ya Dkt Kang’ata kama kiranja wa wengi katika seneti.

Itakumbukwa kuwa mnamo Mei, 2020, Dkt Kang’ata alikuwa mstari wa mbele kuunga mkono kutimuliwa kwa Bi Kihika na Bw Murkomen, bila wao kusomewa makosa yao na kupewa nafasi ya kujitetea mbele maseneta wenzao.

Uamuzi wa kuwatimua wawili hao ulifikiwa katika mkutano wa kundi la maseneta wa Jubilee ulifanyika katika Ikulu ya Nairobi na kuongozwa na Rais Uhuru Kenyatta. Bi Kihika na Bw Murkomen hawakuhudhuria mkutano huo.

Lakini juhudi za wawili hao kupinga kuidhinishwa kwa shoka lililowaangukia ziliambulia patupu katika seneti kutokana na shinikizo kutoka kwa Bw Kang’ata ambaye alishikilia kuwa “huo ni uamuzi wa Rais kama kiongozi wa chama na hauwezi kubatilishwa na yeyote.”

Sawa na ilivyokuwa Mei 2020 ambapo Kang’ata alituma barua za mwaliko kwa maseneta, mwaliko wa mkutano wa kumng’oa Kang’ata ulitumiwa na Naibu wake, Farhiya Haji, ishara kwamba uongozi wa Jubilee ulikuwa umekosa imani na uongozi wake.

Mkutano huo uliongozwa na Katibu Mkuu wa Jubilee Bw Raphael Tuju kwa niaba ya Rais Kenyatta ambaye hakufika. Ingawa Bw Tuju hakutaja jina la Seneta ambaye ameteuliwa kujaza nafasi ya Bw Kang’ata, duru ziliambia Taifa Leo kwamba uongozi wa Jubilee umependekeza nafasi hiyo itunukiwe Seneta wa Kiambu Kimani Wamatangi.

You can share this post!

Uamuzi kortini si tishio kwa ‘Reggae’ – Raila

Maandamano yazuka nchini Sudan kuhusu uchumi, bei za bidhaa