Michezo

Wenger kutuzwa na Rais George Weah Liberia

August 22nd, 2018 1 min read

MASHIRIKA NA CECIL ODONGO

RAIS wa Liberia George Weah anatarajiwa kumzawidi aliyekuwa kocha wa Arsenal, Arsene Wenger na tunu ya rais inayoenziwa sana nchini humo.

Baada ya kutwaa ushindi wa kiti cha urais mwaka 2018, Weah alimwalika Wenger kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwake lakini hilo halikutimia kutokana na majukumu mengi yaliyomzonga mfaransa huyo wakati huo.

Wenger ambaye alikuwa kocha wa Weah mwaka wa 1988 katika klabu ya ufaransa ya Monaco sasa atapokezwa tuzo hiyo maarufu kama Order of Distinction crown katika hafla ambayo siku ya kufanyika kwake bado haijatangazwa na ofisi ya Rais.

“Alinilinda kama mwanawe na bila Arsenal hakuna vile ningepata ufanisi mkubwa katika fani ya soka. Nikikumbuka utiririko wa matukio kutoka siku ya kwanza nilipomwona Monaco, kuibuka mchezaji bora duniani mwaka wa 1995 na kisha kutwaa kiti cha urais, nashukuru sana mwenyezi Mungu,” Rais Weaha aliwahi kunukuliwa akisema.

Ingawa hatua ya Rais Weah imepingwa vikali na baadhi ya raia wa Liberia, serikali yake imefafanua kwamba tuzo hiyo ni ya kutambua juhudi za Wenger katika kuimarisha, kuendeleza fani ya soka katika bara la Afrika na kukuza vipaji vya wachezaji kutoka bara nzima la Afrika katika taaluma yake ya ukufunzi.

Akiwa kocha wa Arsenal, Wenger anatambulika kwa kuwakuza wachezaji 16 kutoka bara la Afrika wakiwemo Nwankwo Kanu, Emmanuel Adebayor na Kolo Toure aliowatumia akiwa Arsenal.