Habari Mseto

Wengi kupoteza ajira National Bank ikinunuliwa na KCB

April 24th, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Huenda watu zaidi wakapoteza kazi katika sekta ya benki kutokana na ongezeko la benki zinazoungana.

Benki ya KCB ndiyo ya hivi punde kutangaza lengo la kununua Benki ya National (NBK).

“Pendekezo la kununua NBK zaidi litaunganisha sekta hiyo na litaimarisha mashirika na kuwezesha KCB kuwa na nafasi kubwa ya kukuza uwezo wa idadi ya watu wanaotumia huduma za benki,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa KCB Joshua Oigara.

Hii ni kuongezea asilimia 30 ya hisa benki hiyo iliyopata Imperial na kuifanya kuwa imara zaidi.

Ingawa mashirika yaliyoimarika ni mazuri, nafasi katika sekta ya benki zitazidi kudidimia. Sekta hiyo ni kati ya sekta ambazo hutoa nafasi zaidi za kazi nchini.

Kuporomoka kwa Chase Bank, Imperial na Dubai zikifuatana kulifanya wafanyikazi wengi kupoteza kazi, na kulazimisha wengi zaidi kuondoka kwenda kutafuta ajira kwingineko.

Data kutoka Benki Kuu ya Kenya inaonyesha kuwa zaidi ya kupoteza kazi kutokana na benki kutofanya vyema, benki zilizosalia zinaendelea kupunguza nafasi za kazi kwa lengo la kukabiliana na gharama kubwa ya operesheni.

Hii ni kutokana na kudhibitiwa kwa viwango vya riba na matumizi ya mfumo wa kidijitali.

Katika muda wa miaka mitatu kufikia Desemba 2017, benki zimefuta kazi wafanyikazi 6,020 na wafanyikazi zaidi huenda wamepoteza kazi mwaka wa 2018 na 2019.