Akili Mali

Wengi Lamu wakimbilia kazi ya kutoa magamba ya samaki

February 4th, 2024 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa Lamu wameibukia mbinu ya kupara samaki kama njia mojawapo ya kujipatia mtaji kukabiliana na hali ngumu ya maisha nchini.

Mbinu hiyo mpya imenoga hasa kwenye visiwa vya Lamu, Shela, Kizingitini, Faza, Mkokoni, Kiwayu, Matondoni na sehemu nyingine.

Aghalabu utawapata wakazi, wakubwa kwa wadogo, wakimiminika kwenye fuo mbalimbali za Bahari Hindi majira ya alfajiri na jioni ilmradi wategee wateja wanaohiari kuwakodisha kupara shehena za samaki kwa malipo.

Mmoja wa watoaji tajika wa huduma ya kupara samaki kisiwani Lamu, Khamis Lali, alisema wao huwatoza wateja wao kati ya Sh50 na Sh100 kuwaparia kilo moja ya samaki.

Kulingana na Bw Lali, wengi wa wanaotoa huduma hiyo hupata fedha nyingi kwa siku, hasa kulingana na bidii ya mtu.

“Kupara samaki sasa kumegeuka kuwa taaluma muhimu kwetu. Hali ngumu ya maisha ndiyo imetusukuma kuingilia kazi hii ambayo imekuwa kitega uchumi cha kutegemeeka kwa wengi wetu. Biashara imenoga vilivyo. Kwa siku mimi sikosi chini ya Sh500,” akasema Bw Lali.

Hussein Twalib anasema yeye binafsi hafikirii kutoka kwenye biashara hiyo ambayo imemwezesha kukimu mahitaji mengi ya familia.

Bw Twalib alianza kujishughulisha na uparaji wa samaki miaka miwili iliyopita.

Anasema wateja wake wengi ni akina mama wanaonunua shehena kubwa kubwa za samaki kutoka kwa wavuvi kila asubuhi na jioni kwa minajili ya kukaranga na kuuza samaki hao.

“Nawashukuru sana hao akina mama. Wengi hunikimbilia wakitaka niwatolee magamba na matumbo ya samaki. Shehena zao huwa ni kubwa kubwa. Mara nyingi wao huishia kuniachia hadi Sh1000 baada ya kuwaparia samaki. Wao hukimbilia kwangu eti kwa sababu ya wepesi wangu katika kuwatayarishia samaki wao,” akasema Bw Twalib.

Baadhi ya wavuvi pia wamejitosa katika huduma ya kupara samaki ili kuongeza pato lao la siku.

Wanaume wakijibanza pembezoni mwa ufuo wa Bahari Hindi eneo la Shella, Kaunti ya Lamu wakipara samaki na kuondoa matumbo. Wakazi wengi wa Lamu wameichangamkia kazi ya kupara samaki kujipatia mtaji kisiwani Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Mmoja wa wavuvi, Safari Kitsao anafafanua kuwa bei ya samaki walioparwa na wale ambao hawajaparwa huwa ni tofauti.

“Kilo ya samaki ambao hawajaparwa huuza kwa kati ya Sh250 na Sh350. Ikiwa mteja ametayarishiwa samaki hao, ikiwemo kuwatoa magamba na matumbo, kilo moja atanunua kwa bei ya juu ya hadi Sh500 kwa kilo. Mbali na kuvua baharini, pia nimekuwa nikipara samaki ili kujiongezea kipato kukabiliana na hali ngumu na ughali wa maisha,” akasema Bw Kitsao.

Kaunti ya Lamu ina zaidi ya wavuvi 7000 ambao mbali na kuvua na kuuzia wateja samaki, pia wamejitosa kwenye biashara ya kuparia wateja hao samaki.