Habari Mseto

'Wengi Nairobi walegeza kuzingatia kanuni za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona'

December 17th, 2020 2 min read

Na SAMMY KIMATU

WAKENYA wengi wamelegeza kuzingatia kanuni zilizowekwa na wizara ya afya kudhibiti msambao wa virusi vya corona.

Jana Jumatano, Taifa Leo ilifanya uchunguzi wake katikati mwa jiji la Nairobi na kubaini kwamba wengi wanapuuza maagizo ya wizara ya afya.

Baadhi ya maeneo kanuni hizo zinapuuzwa ni pamoja na vituo vya magari ya uchukuzi sawia na masoko.

Katika maeneo ya Ngara, Toi, Parklands, Muthurwa, Wakulima na Ladhies baadhi ya wauzaji pamoja na wateja hawazingatii kuweka umbali, wengine hawavalii barakoa na waliovalia waliziteremsha hadi kidevuni.

Isitoshe, baadhi ya mitungi ya maji ya kunawia mikono ilikuwa bila maji sambamba na kukosa sababu pia. Kando na hayo, vinyeyuzi pia vilikuwa vimeadimika. Baadhi ya wafanyabaisahara tuliozungumza nao walikiri kwamba hawawezi kuwachunga wenzao kwani ni jukumu la kila mmoja kuzingatia kanuni hizo.

“Siwezi kumlazimisha mteja wangu kunawa mikono kwani mimi niko kazini kutafuta pesa, ’’ mama mmoja muuzaji wa ndizi katika Soko la Ladhies asema.

Aidha, katika sehemu ya kuuzia nyanya katika Soko la Muthurwa, mambo yalikuwa ni yayo hayo huku wafanyabiashara wakitangamana na wanunuzi bila kuzingatia kuvaa barakoa wala kunawa mikono.

Tuliozungumza nao kuhusu kupuuza kanuni za kuzuia kusambaa kwa corona walisema wamechoka na wengine wakitilia shaka wakidai hawaamini idadi ya maambukizi inayotolewa kila siku na wizara husika.

“Kungekuwa kuna corona hapa sokoni, sioni yeyote ambaye atasazwa bila kuambukizwa wala kuepuka kupelekwa karatini ya lazima,” mama mmoja aliyezungumza kwa sharti asitajwe jina alinena.

Katika kituo cha matatu cha Muthurwa, mitungi michache ya maji iliyokuwepo haikuwa na maji ya kunawia mikono.

Kwingineko katika kituo cha mabasi cha Country Bus, Athusi, Bus Station, Railways na Afya Centre abiria walikuwa wamefurika kuabiri magari bila kuweka umbali. Wengi wao walivalia barakoa zikiwa zimeteremsha hadi kidevuni.

“Watu wanang’ang’ania matatu angalau wasafiri mashambani bila kujali wakiepuka kukwama jijini wakihofia nauli itapanda tunapokaribia Sikukuu ya Krismasi,” Bw Jonathan Musau akasema.

Hata hivyo, katika steji ya mabas ya Kencom na Ambassadeur, hakuna abiria aliruhusiwa kuabiri bas bila kunawa wala kutumia kinyeyuzi pamoja na kupimwa viwango vya joto.

“Ni sheria kwa Sacco yetu kuzingatia kanuni zifaazo la sivyo hili gari litapigwa marufuku na wasimamizi wetu wacha vile mnaweza maafisa wa polisi au maafisa wa afya. Hapa mambo huchukuliwa kwa uzito,” dereva wa mabasi ya ‘Double M’ akasema.

Kuna visa vya ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona katika wimbi la pili ikilinganishwa na wimbi la kwanza tangu kuripotiwa kwa kisa cha kwanza cha corona mnamo Machi 13, 2020, nchini Kenya.