Habari

Wenye hoteli wasihi Uhuru asifunge nchi

December 11th, 2020 2 min read

Na WINNIE ATIENO

WAWEKEZAJI katika sekta ya utalii wamewaonya magavana dhidi ya hatua ya kumshinikiza Rais Uhuru Kenyatta kuweka sheria ya kufungia watu maeneoni yao kufuatia kuongezeka kwa virusi vya corona nchini.

Aidha magavana walidokeza kwamba wanapania kuzuia watu kusafiri wakati wa sherehe za krismasi na mwaka mpya.

Kaunti zinazolengwa kufuatia kuongezeka kwa virusi ni pamoja na Nairobi, Mombasa, Kiambu, Nakuru, Kajiado, Uasin Gishu, Busia, Machakos, Kisumu na Kilifi.

Magavana wana wasiwasi kwamba Wakenya wanaosafiri kusherehekea Krismasi na Mwaka Mpya watasababisha kuenea zaidi kwa corona.

Hata hivyo, wawekezaji wa sekta ya utalii ambayo imeyumbishwa na janga la corona wamewashutumu magavana kwa hatua hiyo huku wakiipiga vikali.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa wawekezaji wa utalii nchini Bw Mohamed Hersi, wamesema hatua ya magavana ni hatari.

“Tusikubali magavana wapitishe hoja hii. Baraza la magavana linafaa kushughulikia namna ya kudhibiti maambukizi kwa kuweka sehemu ya wagonjwa wa corona na kuwapa wahudumu wa afya vifaa vya kupambana na ugonjwa huu,” alisema Bw Hersi.

Alisema magavana wengi hawajaweka mikakati bora ya kupambana na janga hilo.

“Mkurugenzi mmoja wa maswala ya mawasialiano aliaga dunia katika kaunti moja nchini sababu ya kukosa hewa ya oksijeni katika hospitali moja. Yeyote anayeshinikiza serikali kuweka lockdown nyingine ana mzaha. Lazima tushughulikie swala la afya na namna ya Wakenya wanavyojimudu. Virusi viko miongoni mwa jamii na kote nchini,” alisisitiza.

Bw Hersi alimsihi Rais Kenyatta kupuuza matakwa ya magavana hao badala yake akiwataka magavana kuhakikisha sheria za kukabiliana na janga hilo zinahimizwa.

“Hawa magavana wanaoshinikiza kuwekwe ‘lockdown’ watapata idhini ya kusafiri sehemu yoyote nchini. Tupinge azma yao. Watumie muda na nguvu zao kusuluhisha mgomo unaonuiwa wa madaktari. Wahakikishe madaktari wanalipwa, mbona wasilipwe?” aliuliza.

Haya yanajiri siku chache baada ya wamiliki wa mahoteli ya kifahari eneo la Pwani kuisihi serikali kutofunga nchi wakisema utalii umeathirika pakubwa na janga la corona.

Walisema Krsimasi ya mwaka huu inaonyesha namna utalii umeathirika baada ya wageni wachache kuanza safari zao kwenye hoteli za Pwani.

Aidha, alilaumu wasiwasi wa wakenya dhidi ya mpango wa serikali kufunga nchi ili kupunguza maambukizi huku wakimtaka Rais Kenyatta kutofunga nchi.

Takwimu za hivi karibuni, zinaonyesha Kenya imepoteza asilimia wageni 72 wa kimataifa kwa kipindi cha miezi 10 ikilinganishwa na mwaka jana kufuatia janga la corona.

Kulingana na takwimu kutoka shirika la utafiti wa utalii nchini, Kenya ilinakili wageni 470,971 kati ya Januari hadi Oktoba mwaka huu ikilinganishwa na wageni 1,718,155 wa kimataifa mwaka 2019.