Wenye makalio makubwa wana akili ndogo – Utafiti

Wenye makalio makubwa wana akili ndogo – Utafiti

MASHIRIKA Na PETER MBURU

WANASAYANSI wamechapisha utafiti ambao unaweza kuzua pingamizi kali, baada yao kubaini kuwa watu walio na nyama nyingi katika sehemu ya makalio wana akili ndogo.

Kulingana na utafiti huo ambao ulichapishwa Januari 9 katika jarida la Neurology, watu wanene kiunoni wana uchache wa chembechembe za ‘gray matter’ kwenye akili, ambazo kwa kawaida hubeba bilioni 100 ya mishipa kwenye akili.

Watafiti hao walisema kuwa unene wa mwili ulidhihirisha kuchangia kupungua kwa upevu wa akili katika maeneo manne.

Utafiti huo ulihusisha watu 9,652 wa umri wa makamo Uingereza, ambapo uzito wa mwili-ukilinganishwa na urefu (BMI) na ukubwa wa kiuno hadi mapajani ulipimwa. Kisayansi, kipimo cha kati ya 18.5 na 24.9 cha BMI huwa salama kiafya, lakini kikizidi 30 mtu anaweza kuitwa mnene kupita kiasi.

Kulingana na vigezo walivyotumia wanasayansi hao, mmoja kati ya kila wahusika 5 wa utafiti huo walipatikana kuwa wanene kupita kiasi.

Watafiti hao aidha walitumia teknolojia kupima upevu wa akili wa wahusika, wakizingatia umri, namna mwili unafanyishwa kazi, uvutaji wa sigara ama ugonjwa wa kupanda damu. Walibaini kuwa watu walio na kiwango cha juu cha vipimo vya BMI (unene mkubwa ikilinganishwa na urefu wa mwili), ama ukubwa kiunoni walikuwa na kiwango kidogo cha chembe chembe za ‘gray matter’ akilini.

“Upungufu wa ukubwa wa akili unaongezeka kadri mafuta katika sehemu ya kiuno yanazidi kuongezeka,” akasema mkuu wa utafiti huo Hamer.

Katika idadi halisia, watu 1,291 ambao walikuwa na kiwango cha BMI cha zaidi ya 30 na ukubwa kwenye sehemu za kiuno na mapaja walipatikana kuwa na kiwango kidogo sana cha chembechembe za gray matter akilini, kikiwa sentimita 786 mraba, watu 514 ambao walikuwa na kiwango cha BMI zaidi ya 30 lakini hawakuna wanene sehemu ya kati ya mwili nao walikuwa na kiwango cha gray matter kwa kadiri, kikiwa sentimita 798 mraba.

Utafiti huo ulihusisha unene mkubwa wa mwili na kufinyika kwa sehemu fulani za akili kama pallidum, nucleus accumbens, putamen (ambayo huhusishwa na kiwango cha juu cha BMI) na caudate (ambayo huhusishwa na ukubwa kiunoni).

“Haifahamiki ikiwa hali hiyo katika akili ndiyo huchangia unene wa mwili ama ni unene wa mwili unaopelekea akili kuwa hivyo,” akasema Prof Hamer.

Utafiti huo ulishauri watu kufanya bidii kuwa katika hali nzuri ya mwili kiafya na kuhakikisha hawawi na uzito mkubwa.

You can share this post!

Afisa wa KDF taabani kuhusu hongo ya kuingiza vijana kwa...

Teknolojia ya 5G kutetemesha mitandao 2019

adminleo