Habari

Wenye mshahara mnono kukatwa ushuru wa juu

May 17th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

WATU binafsi na kampuni zinazopata mapato ya juu zaidi nchini wameongezewa ushuru wa asilimia 35 huku Hazina ya Fedha ikilenga kuimarisha viwango vya mapato ya serikali.

Hazina hiyo inalenga kuongeza kiwango cha mapato yanayotokana na ushuru hadi Sh68 bilioni.

Katika mswada mpya uliowasilishwa Bungeni na Waziri wa Fedha Henry Rotich, mpango huo unalenga watu wanaopata Sh9 milioni kwa mwaka.

Hii ni kumaanisha, wote wanaopata Sh750, 000 na zaidi kwa mwezi wanalengwa na mswada huo.

Hata hivyo, idadi ya watu wanaopata kiasi hicho cha fedha ni ndogo mno ikizingatiwa kuwa watu wengi hufanya kazi na serikali na hupata Sh57,915 kwa mwezi kiwango cha wastani.

Wanaofanya katika sekta ya kibinafsi hupata Sh56,624 kwa mwezi kiwango cha wastani kulingana na utafiti wa kiuchumi wa 2018.

Pia, mswada huo unalenga kampuni ambazo hupata faida ya Sh500 milioni kila mwaka.