Were aongoza Zesco United kutesa ligini Zambia NAPSA Stars anayochezea Calabar yabwagwa

Were aongoza Zesco United kutesa ligini Zambia NAPSA Stars anayochezea Calabar yabwagwa

Na GEOFFREY ANENE

ZESCO United imeendelea kutetemesha kwenye Ligi Kuu ya Zambia baada ya kuchabanga Lumwana Radiants 4-1 katika mechi ambayo Wakenya Ian Otieno (kipa) na Jesse Were (mshambuliaji) walianza Alhamisi.

Vijana wa Numba Mumamba walicheka na nyavu za Lumwana kupitia wachezaji Adrian Chama dakika ya saba, Solomon Sakala (46), Luwawa Kasoma (63) na Thabani Kamusoko (90+2).

Chama alivuta kombora safi kutoka katikati mwa uwanja hadi wavuni baada ya kuona kipa Ngelewa Katembwa akiwa amesonga mbali na lango. Were alipoteza nafasi nzuri dakika ya 15 baada ya pasi za nipe nikupe na Winston Kalengo.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu ya Tusker FC kisha alichanja kona murwa iliyozalisha bao la pili. Alipumzishwa dakika ya 50 wakati Numba alijaza nafasi yake, ile ya Tafadzwa Rusike na Chanda Mukuka kwa kuingiza John Ching’andu, Donashano Malama na Luwawa Kasoma. Kasoma alipokea pasi nzuri kutoka kwa Kalengo akipachika bao lake.

Otieno kisha alikubali nyavu zake kuchanwa aliposukumiwa kiki kali na Emmanuel Manda ambalo hakuweza kupangua dakika ya 71. Kamusoko, Enock Sakala na Ching’andu walipanga soka safi iliyozalisha goli la nne.

Alama tatu zilitosha kurejesha Zesco juu ya jedwali la ligi hiyo ya timu 18 ikiwa imezoa jumla ya alama 37 baada ya kushuka uwanjani mara 19. Imefungua mwanya wa alama moja dhidi ya nambari mbili Zanaco ambayo imecheza michuano 20.

Lusaka Dynamos, ambayo imeajiri Wakenya Musa Mohammed na Duncan Otieno, ilipoteza mechi yake ya pili mfululizo ilipolimwa 3-0 na Forest Rangers mnamo Jumatano, ina alama 30 kutokana na michuano 20.

NAPSA Stars wanayochezea beki David ‘Calabar’ Owino Odhiambo na kipa Shaaban Odhoji, iko nje ya mduara hatari wa kutemwa kwa tofauti ya magoli na Young Green Eagles inayokamata nafasi ya 15 kwa alama 21.

Timu ya NAPSA ilicharazwa 3-1 na Young Green Eagles mnamo Alhamisi. Calabar alitumiwa kama mchezaji wa akiba akiingia nafasi ya Bornwell Silengo dakika 76. Odhoji alikuwa benchi.

Mabingwa watetezi Nkana wako ndani ya maeneo ya kushushwa ngazi katika nafasi ya 16 kwa alama 20 baada ya kujibwaga uwanjani mara 17. Nkana walizabwa 2-0 na Kabwe, kichapo hicho kikiwa ni cha tatu mfululizo ligini. Nkana imeajiri kiungo mshambuliaji Mkenya Duke Abuya.

  • Tags

You can share this post!

Bakken Bears anayochezea Tylor Ongwae yapigwa breki baada...

Echesa anaswa akimzaba kofi afisa wa IEBC katika uchaguzi...