Michezo

Were na Akumu wachangia Zesco kuchapa Zanaco 1-0

September 2nd, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA Jesse Were na Anthony Akumu walishiriki mechi ya ufunguzi ya Ligi Kuu klabu yao ya Zesco United ikichapa Zanaco 1-0 uwanjani Levy Mwanawasa mnamo Agosti 31, 2019.

Mabingwa watetezi Zesco, ambao walikuwa wamelimwa 4-1 walipokutana na Zanaco mara ya mwisho Aprili 20 mwaka 2019, walipata bao la ushindi kutoka Enock Sabumukama.

Zesco, ambayo pia imeajiri beki Mkenya David Owino, nambari 16 itakutana na Nakambala Leopards katika mechi yake ijayo mnamo Septemba 14.

NAPSA Stars inaongoza ligi hii ya klabu 18 kwa alama tatu baada ya kulipua Mufulira 2-0.

Buildcon ni ya pili baada ya kulima Kysa 2-1 mjini Kabwe. Red Arrows, Nkwazi na Kansanshi pia zimevuna alama tatu baada ya kubwaga Nakambala Leopards, Forest Rangers na Power Dynamos kwa bao 1-0 mtawalia.

Kabwe Warriors na Green Eagles zinashikilia nafasi ya saba kwa pamoja baada ya kuagana 1-1.