Michezo

Were na Tololwa waona lango Zesco na Red Arrows zikitamba

September 22nd, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MSHAMBULIAJI Jesse Were alifunga bao lake la nne katika mechi mbili na kusaidia Zesco United FC kunyamazisha wageni Lumwana Radiants FC katika mechi ya Ligi Kuu ya Zambia uwanjani Levy Mwanawasa, Jumamosi.

Were alifungua ukurasa wa magoli dakika ya 31, lakini timu hizi zilienda mapumzikoni bega kwa bega 1-1 baada ya Lumwana kujibu kupitia kwa Emmanuel Manda kutokana na kona.

Thambani Kamusoko alipachika bao la ushindi la Zesco dakika ya 79 kupitia ikabu.

Mbali na Were, kiungo Anthony Akumu na beki David Owino pia kutoka Kenya, walishiriki mchuano huu.

Ushindi huu ni wa tatu mfululizo wa Zesco msimu huu. Were alifunga mabao matatu, moja kupitia penalti, Zesco ikizaba Nakambala Leopards mnamo Septemba 18. Kabla ya hapo, Zesco, ambayo inaongoza ligi hii ya klabu 18, ilikuwa imefungua msimu kwa kuliza Zanaco 1-0 Agosti 31.

Naye mchezaji wa zamani wa AFC Leopards, Andrew Tololwa alifungia Red Arrows bao la ushindi ikipiga Power Dynamos 2-1.

Linos Makwaza aliweka Dynamos kifua mbele dakika ya 30 kabla ya Red Arrows kujibu katika kipindi cha pili kupitia kwa James Chamanga dakika ya 65 naye Mkenya Tololwa, ambaye aliingia kama mchezaji wa akiba, akahitimisha dakika ya 89. Ushindi huu ni wa pili mfululizo wa Red Arrows dhidi ya Dynamos ligini.

Red Arrows inashikilia nafasi ya pili nyuma ya Zesco kwa ubora wa magoli baada ya kubwaga Lumwana Radiants na Nakambala Leopards kwa bao 1-0 kila mmoja katika mechi mbili za kwanza.

Wakenya Harun Shakava na Duncan Otieno wametajwa katika kikosi cha Nkana FC kitakachovaana na Mufulira Wanderers baadaye leo. Nahodha wa zamani wa Gor Mahia, Shakava ametiwa katika kikosi kitakachoanza mechi hiyo naye kiungo wa zamani wa AFC Leopards, Otieno ametiwa kitini.

Matokeo na ratiba:

Septemba 21

Buildcon 2-2 Forest Rangers

Nkwazi 3-2 Zanaco

Green Eagles 3-2 Nakambala Leopards

Kabwe Youth Academy 2-2 Kabwe Warriors

Kansanshi 1-0 Green Buffaloes

Red Arrows 2-1 Power Dynamos

Zesco United 2-1 Lumwana Radiants

Septemba 22

Lusaka Dynamos na Napsa Stars

Nkana na Mighty Mufulira Wanderers