Michezo

West Brom wamfuta kazi kocha Bilic kutokana na matokeo duni

December 16th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

WEST Bromwich Albion wamemfuta kazi kocha Slaven Bilic baada ya kudhibiti mikoba yao kwa kipindi cha miezi 18.

Kutimuliwa kwa Bilic kunajiri baada ya matokeo duni ambayo yameshuhudia kikosi cha West Brom kikishuka hadi nafasi ya 19.

Hadi kufikia sasa, West Brom, wamejizolea alama saba kutokana na mechi 13 za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ambapo wamepoteza mechi nane licha ya kuwalazimishia miamba Manchester City sare ya 1-1 mnamo Disemba 15, 2020.

Mbali na Bilic, 52, wakufunzi wengine ambao wametimuliwa na West Brom ni waliokuwa wasaidizi wake – Dean Racunica, Danilo Butorovic na Julian Dicks.

Bilic alitia saini mkataba wa miaka miwili alipopokezwa mikoba ya West Brom almaarufu ‘The Hawthorns’ mnamo Juni 2019 baada ya kuaminiwa fursa ya kumrithi Darren Moore.

Chini ya usimamizi wake, West Brom walifuzu kushiriki kivumbi cha EPL msimu huu wa 2020-21 baada ya kukamilisha kampeni za Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Uingereza (Championship) katika nafasi ya pili mnamo 2019-20.

Hata hivyo, kikosi hicho kimesajili ushindi mara moja pekee kwenye EPL hadi kufikia sasa msimu huu baada ya kupepeta Sheffield United 1-0 mnamo Novemba 28, 2020.

Mechi ya Disemba 15, 2020 iliyokutanisha West Brom na Man-City ilikuwa ya 100 kwa Bilic ambaye ni raia wa Croatia kusimamia kwenye kampeni za EPL.

Kocha huyo amewahi pia kudhibiti mikoba ya West Ham United kati ya Juni 2015 na Novemba 2017. Wakati huo, alisaidia kikosi hicho kukamilisha kampeni za EPL katika nafasi ya saba, hiyo ikiwa nafasi nzuri zaidi kwa kikosi hicho kuwahi kufikia kwenye historia ya EPL tangu 2002.

Kabla ya hapo, aliwahi kuwaongoza Croatia kufuzu kwa fainali mbili za Euro na kikosi hicho kikatinga robo-fainali za Euro 2008 baada ya kuwabandua Uingereza kwenye mchujo.

Bilic amewahi pia kuhudumu kama kocha katika vikosi vya Hajduk Split, Lokomotiv Moscow, Besiktas na Al-Ittihad.

Sam Allardyce, Nigel Pearson, Mark Hughes na Eddie Howe ndio makocha wanaopigiwa upatu wa kupokezwa mikoba ambayp Bilic amepokonywa kambini mwa West Brom.

Allardyce hajawahi kupata klabu ya kufunza tangu aagane na Everton mnamo 2018, mwaka ambao ulimshuhudia pia Hughes akikatiza uhusiano na Southampton.

Pearson, aliwahi kushikilia mikoba ya West Brom, aliongoza Watford kwenye mechi 20 za EPL mnao 2019-20 kabla ya kufutwa huku Howe akibanduka kambini mwa Bournemouth mnamo Agosti baada ya kikosi chake kushushwa ngazi kwenye EPL.