Michezo

West Ham kuwatema Zabaleta na Sanchez

June 26th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

WEST Ham United wamethibitisha kwamba wanasoka Pablo Zabaleta na Carlos Sanchez wataagana nao kirasmi mwishoni mwa Juni 2020.

Beki chipukizi Jeremy, Ngakia, 19, pia atabanduka kambini mwa West Ham baada ya kukataa kile ambacho kikosi hicho kimesema ni “ofa nzuri ya kuvutia”.

Kuondoka kwa Ngakia kutakuwa pigo kubwa kwa kocha David Moyes ambaye alimtegemea pakubwa katika kikosi alichokiwajibisha dhidi ya Wolves mnamo Juni 20, 2020.

Hata hivyo, tineja huyo anayehusishwa na uwezekano mkubwa wa kutua Watford, hakuwa sehemu ya kikosi cha West Ham kilichobamizwa na Tottenham 2-0 mnamo Juni 23, 2020.

“Kwa mujibu wa sera za klabu, Ngakia alipokezwa ofa bora kutokana na ufanisi wake wa kuingia katika kikosi cha kwanza mwanzoni mwa mwaka huu. Isitoshe, alipata uhakika wa muda wa kucheza katika takriban kila mchuano, na hili ni jambo ambalo lingemkuza sana kitaaluma,” ikasema sehemu ya taarifa ya West Ham.

“Hata hivyo, Ngakia na mawakala wake walikataa ofa waliyopokezwa na wakatupilia mbali pendekezo la kurefushwa kwa mkataba wake kwa kipindi kifupi hadi mwishoni mwa msimu huu,” ikaendelea taarifa hiyo.

Zabaleta, 35, alikuwa na mkataba mpya uliokuwa utamatike rasmi mwishoni mwa msimu huu. Hata hivyo, jeraha jipya alilolipata mwanzoni mwa mwaka huu lilimnyima fursa ya kurefusha muda wa kuhudumu kwake uwanjani London.

Kwa upande wake, Sanchez, 34, amewajibishwa katika mchuano mmoja pekee wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.