Michezo

West Ham njiani wakielekea Championship

June 24th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

TOTTENHAM Hotspur walisajili ushindi wao wa kwanza baada ya mechi nane za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Juni 23 na kuwaacha West Ham United katika hatari ya kuteremshwa ngazi mwishoni mwa msimu huu.

Kiungo mzawa wa Jamhuri ya Czech, Tomas Soucek alijifunga kutokana na kona iliyochanjwa na Giovani lo Celso kunako dakika ya 64 kabla ya Harry Kane kucheka na nyavu za wageni wao katika dakika ya 82 na kusaidia kikosi chao kuvuna ushindi wa 2-0. Bao la Kane lilikuwa lake la 18 hadi kufikia sasa katika EPL muhula huu.

Zikisalia mechi saba pekee kabla ya kampeni za EPL msimu huu kutamatika rasmi, West Ham wamejipata ndani ya mduara wa vikosi vilivyopo katika hatari ya kushushwa ngazi kwa pamoja na Bournemouth, Aston Villa na Norwich City. Hatari zaidi kwa West Ham ya kocha David Moyes ni kwamba wao wamecheza mechi moja zaidi kuliko vikosi hivi vingine mkiani mwa jedwali.

Licha ya kujitahidi kurejea mchezoni, kisu cha makali ya West Ham kilisalia butu kwa kipindi kizima cha mchezo japo Jarrod Bowen alishuhudia kombora lake likigonga mwamba wa goli la Spurs mwishoni mwa kipindi cha pili.

Ushindi wa Spurs ambao kwa sasa wananolewa na kocha Jose Mourinho, uliwapaisha hadi nafasi ya saba kwa alama 45 jedwalini. Ni pengo la alama sita pekee ndilo linalotamalaki kati yao na Chelsea wanaofunga orodha ya nne-bora.

Mchuano huo ulikuwa wa 300 kwa Mourinho kusajili ushindi kwenye soka ya Uingereza. Spurs kwa sasa wamejizolea alama nne kutokana na mechi mbili za nyumbani dhidi ya Manchester United na West Ham United.

Tottenham kwa sasa wanajiandaa kuwaendea Sheffield United uwanjani Bramall Lane mnamo Julai 2 huku West Ham wakiwaalika Chelsea kwa gozi jingine la jiji la London mnamo Julai 1, 2020.