West Ham United wajinasia huduma za Danny Ings kutoka Aston Villa

West Ham United wajinasia huduma za Danny Ings kutoka Aston Villa

Na MASHIRIKA

WEST Ham United wamemsajili mshambuliaji Danny Ings kutoka Aston Villa kwa Sh2.3 bilioni.

West Ham wamelipa kwanza kima cha Sh1.8 bilioni kwa ajili ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 30. Kiasi hicho cha pesa kitafikia Sh2.3 bilioni iwapo kikosi hicho cha kocha David Moyes kitakosa kushuka ngazi kwenye kipute cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) muhula huu wa 2022-23.

West Ham walikamilisha uhamisho wa Ings kufikia alasiri ya Januari 20, 2023 na sogora huyo raia wa Uingereza anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi kitakachowajibishwa na West Ham dhidi ya Everton mnamo Januari 21, 2023 ugani London Stadium.

Ings anaingia katika sajili rasmi ya West Ham kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kuhudumu kambini mwa Villa kwa miezi 18. Alijiunga na Villa mnamo Agosti 2021 baada ya kuagana na Southampton kwa Sh3.9 bilioni.

Kusajiliwa kwake kulichochewa na ulazima wa West Ham kujaza pengo la Gianluca Scamacca anayetarajiwa kusalia mkekani kwa muda mrefu kuuguza jeraha la goti. Kuumia kwa Scamacca kuliacha Michail Antonio akiwa mshambuliaji wa pekee tegemeo kambini mwa West Ham ambao sasa ni miongoni mwa vikosi vitatu vinavyovuta mkia kwenye jedwali la EPL.

Ni Wolverhampton Wanderers pekee ambao wana chini ya mabao 15 ambayo yamefungwa na West Ham kufikia sasa katika EPL msimu huu. West Ham hawajashinda mechi saba zilizopita za EPL.

Ings anaingia kambini mwa West Ham akijivunia kufunga mabao saba kutokana na mechi 21 zilizopita japo hajawajibishwa katika mchuano wowote tangu fainali za Kombe la Dunia za 2022 zikamilike nchini Qatar mnamo Disemba 18, 2022.

Ana mabao sita katika EPL msimu huu, moja zaidi kuliko ambayo Antonio na Scamacca wamejivunia kufikia sasa. Antonio na Scamacca walifunga bao kila mmoja katika ushindi wa 3-1 uliosajiliwa na West Ham dhidi ya Fulham mnamo Oktoba 9, 2022.

Isipokuwa majeraha mengi yaliyomtatiza akivalia jezi za Liverpool, Ings ni fowadi wa kutegemewa katika safu ya mbele huku akipachika wavuni wastani wa bao moja kila baada mechi tatu tangu aanze kuchezea Burnley, Southampton na Villa. Mechi yake ya mwisho akivalia jezi za Villa ilikuwa Novemba 13, 2022 dhidi ya Brighton.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Riggy G akutana na wabunge wa Jubilee kutoka Mlima Kenya...

EPL: Wikendi ya kufa kupona

T L