West Ham United wamvizia Jesse Lingard kutoka Manchester United

West Ham United wamvizia Jesse Lingard kutoka Manchester United

Na MASHIRIKA

WEST Ham United wamefichua mpango wa kusajili upya kiungo mvamizi wa Manchester United, Jesse Lingard.

Nyota huyo raia wa Uingereza mwenye umri wa miaka 29 atasalia mchezaji huru asiye na klabu yoyote mnamo Julai 1 mkataba wake utakapokamilika ugani Old Trafford.

Lingard aliridhisha sana alipokuwa akichezea West Ham kwa mkopo kutoka Man-United mnamo 2020-21 na akafunga mabao tisa kutokana na mechi 16 za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Hata hivyo, alinyimwa kipindi kingine cha mkopo mnamo Januari 2022 baada ya Man-United kukataa kushirikiana na West Ham waliokuwa washindani wao wakuu kwenye vita vya kufuzu kwa soka ya Europa League.

Lingard anatarajiwa kuwa mchezaji wa pili kusajiliwa na West Ham muhula huu baada ya kipa Alphonse Areola kutoka Paris St-Germain (PSG).

West Ham wameafikiana na PSG kuhusu uhamisho wa Areola aliyehudumu ugani London Stadium kwa mkopo mnamo 2021-22. Uhamisho wake utagharimu West Ham ya kocha David Moyes kima cha Sh1.6 bilioni.

Areola aliwajibishwa na West Ham katika mechi zote za Europa League mnamo 2021-22 hadi walipodenguliwa na Eintracht Frankfurt ya Ujerumani kwenye hatua ya nusu-fainali. Sasa anatarajiwa kupigania nafasi na Lucasz Fabianski katika kikosi cha kwanza ligini. Fabianski ambaye ni kipa wa zamani wa Arsenal, alirefusha mkataba wake kwa mwaka mmoja zaidi kambini mwa West Ham mnamo Mei 2022.

West Ham walianza kujiandaa kwa kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu ujao wa 2022-23 mnamo Juni 27, 2022 kwa kuyoyomea Scotland ambapo watapiga kambi ya mazoezi ugani St Andrews.

Watafahamu wapinzani wao kwenye mchujo wa kufuzu kwa kipute kipya cha Europa Conference League mnamo Agosti 1, 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Mashine za kisasa kuifanya kazi ya upanzi wa mboga...

Rooney kurudi shule kusomea ukocha baada ya kuondoka Derby...

T L