West Ham wadengua Man-United kwenye raundi ya tatu ya Carabao Cup

West Ham wadengua Man-United kwenye raundi ya tatu ya Carabao Cup

Na MASHIRIKA

WEST Ham United walilipiza kisasi dhidi ya Manchester United kwa kuwapiga 1-0 na hivyo kuwadengua kwenye raundi ya tatu ya Carabao Cup msimu huu mnamo Jumatano usiku ugani Old Trafford.

Chini ya kocha David Moyes, West Ham walicharaza Man-United siku tatu pekee baada ya mkufunzi Ole Gunnar Solskjaer kuongoza masogora wake kupepeta West Ham 2-1 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani London Stadium.

Licha ya wanasoka Bruno Fernandes na Mason Greenwood kuletwa ugani katika kipindi cha pili, mikakati hiyo ya Solskjaer ilikosa kuzaa matunda.

Bao la Lanzini lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Ryan Fredericks aliyetatiza pakubwa mabeki wa Man-United waliotegemea zaidi maarifa ya Jadon Sancho na Alex Telles.

Andriy Yarmolenko, Mark Noble na Jarrod Bowen ni wanasoka wengine wa West Ham waliojituma zaidi dhidi ya Man-United walioshindwa nyumbani kwa mara ya kwanza tangu 2007 chombo chao kilipozamishwa na Carlos Tevez katika mchuano wa EPL.

Ushindi wa West Ham ulikuwa wao wa kwanza dhidi ya Man-United kwenye kivumbi kisichokuwa cha ligi tangu 2001 walipotambishwa na Paolo di Canio kwenye Kombe la FA.

West Ham walizima matumaini ya Man-United na Solskjaer kutwaa taji la Carabao Cup walilolinyanyua kwa mara ya mwisho mnamo 2017.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Real Madrid waponda Mallorca na kurejea kileleni mwa...

Majangili wavamia kituo na kuiba bunduki